Trump aendeleza bwabwaja zake dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i41956-trump_aendeleza_bwabwaja_zake_dhidi_ya_iran
Rais Donald Trump wa Marekani jana Jumanne alikutana na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia katika Ikulu ya White House na kukariri tena madai yasiyo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 21, 2018 00:36 UTC
  • Trump aendeleza bwabwaja zake dhidi ya Iran

Rais Donald Trump wa Marekani jana Jumanne alikutana na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia katika Ikulu ya White House na kukariri tena madai yasiyo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Katika mazungumzo yake na Muhammad bin Salman, Trump alidai kuwa mienendo ya Iran katika Mashariki ya Kati na duniani kote haifai. 

Donald Trump pia ameashiria mikataba mikubwa ya mauzo ya silaha za Marekani kwa Saudi Arabia na kusema: Marekani ina hamu ya kuiuzia silaha zaidi serikali ya Riyadh.

Mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman aliwasili jana nchini Marekani kwa safari ya wiki mbili na kulakiwa kwa maandamano makubwa ya Wamarekani wanaolaani mauaji ya raia wa Yemen hususan wanawake na watoto wadogo. Tangu kijana huyo mwanagenzi wa siasa alipoteuliwa na baba yake kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia tarehe 21 Juni mwaka jana amekuwa akihudumia kwa nguvu zake zote maslahi ya Marekani na utawala haramu wa Israel.

Sambamba na safari hiyo ya Muhamamd bin Salman nchini Marekani, Baraza la Senati la nchi hiyo limeunga tena mkono mashambulizi yanayofanwya na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya watu wa Yemen. 

Watoto wa Yemen ndio wahanga wakuu wa mashambulizi ya Saudia

Zaidi ya raia elfu 14 wa Yemen wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimishwa kuwa wakimbizi kutokana na hujuma na mashambulizi ya pande zote yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia na washirika wake wakiungwa mkono na Marekani, Israel na Uingereza dhidi ya raia wasio na hatia. 

Nchi hizo mbili za Marekani na Saudi Arabia na utawala haramu wa Israel pia zilikuwa washirika wakubwa wa makundi ya kigaidi hususan Daesh katika nchi za Iraq na Syria.