Ufaransa yapewa miezi miwili isitishe uuzaji wa silaha kwa Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i42050-ufaransa_yapewa_miezi_miwili_isitishe_uuzaji_wa_silaha_kwa_saudia
Mashirika mawili ya kutetea haki za binadamu yameipa Ufaransa makataa ya miezi miwili iache kuuuzia silaha utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, vinginevyo yataichukulia hatua za kisheria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 23, 2018 02:46 UTC
  • Ufaransa yapewa miezi miwili isitishe uuzaji wa silaha kwa Saudia

Mashirika mawili ya kutetea haki za binadamu yameipa Ufaransa makataa ya miezi miwili iache kuuuzia silaha utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, vinginevyo yataichukulia hatua za kisheria.

Mashirika hayo ya Ufaransa ya Droit Solidarite na Aser yamesema serikali ya Paris inakiuka sheria za kimataifa kwa kuiuzia Saudia na Umoja wa Falme Kiarabu silaha zinazotumika katika mashambulizi ya anga dhidi ya wananchi wa Yemen.

Benoit Muracciole, Rais wa shirika la Aser ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, "Ufaransa haiheshimu sheria za kimataifa na iwapo haitatii muhula tulioutoa, basi tutaishtaki kwa Conseil d’Etat, mamlaka ya juu zaidi ya masuala ya sheria nchini."

Tayari mashirika hayo yamemuandikia barua Edouard Phillipe, Waziri Mkuu wa Ufaransa wakimtaka abatilishe mara moja leseni za kuziuzia silaha Saudia na Imarati.

Sehemu ndogo ya hujuma za anga za Saudia dhidi ya Yemen

Hii ni katika hali ambayo, leo Ijumaa shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema mauzo ya silaha za nchi za Magharibi kwa Saudia na waitifaki wake zinazotumika katika hujuma dhidi ya Yemen ni kejeli kwa Makubaliano ya Kimataifa ya Uuzaji wa Silaha.

Saudia kwa kushirikiana na Marekani,  utawala haramu wa Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu, ilianzisha mashambulizi ya kila upande dhidi ya taifa masikini la Yemen hapo mwezi Machi 2015, ambapo mbali na kuua makumi ya maelfu ya watu, yameharibu miundombinu ya nchi hiyo maskini.