Pakistan yaionya Marekani kwa kuyawekea vikwazo mashirika yake saba ya nyuklia
Serikali ya Pakistan imetoa radiamali ya onyo kwa Marekani kufuatia hatua ya Washington ya kuyawekea vikwazo mashirika saba ya nchi hiyo kwa kujihusisha na shughuli za nyuklia.
Muhammad Faisal, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan ametangaza kwamba, vikwazo hivyo vya Marekani dhidi ya mashirika hayo ya Pakistan, vinatokana na sababu za kisiasa. Ameongeza kwamba, Pakistan inaendelea kuchunguza suala la kuwekewa vikwazo mashirika saba ya nchi hiyo kwa kile kilichotajwa na Washington kuwa ni kujihusisha na shughuli hatari za biashara ya nyuklia.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan amesisitiza kuwa, Islamabad imekuwa ikitekeleza jukumu la kutoeneza silaha za nyuklia na kwamba, kile kilichotekelezwa na Washington kuhusiana na vikwazo, hakitakiwi kufanywa kwa sababu za kisiasa. Inafaa kuashiria kuwa, serikali ya Marekani imeyawekea vikwazo mashirika saba ya Pakistan kutokana na mashirika hayo kufanya biashara katika sekta ya nyuklia na kwa kisingizio cha usalama wa taifa na maslahi ya kisiasa ya Marekani.
Vyombo vya habari nchini Pakistan vimeripoti kwamba, lengo la vikwazo hivyo ni kushadidisha mashinikizo dhidi ya Islamabad kutoka kwa serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani. Washington imedai kwamba mashirika hayo yamekuwa yakiendesha shughuli hatari za nyuklia kwa uwazi na kwamba suala hilo linatishia usalama wa taifa na maslahi ya kisiasa ya Marekani.
Uhusiano wa Washington na Islamabad umeingia doa tangu Trump alipotamka kwamba Pakistan ni kitovu cha ugaidi.