Apr 04, 2018 14:26 UTC
  • Cuba: Jinai za Israel dhidi ya Wapalestina ni ukiukaji wa haki za binadamu

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Cuba imetoa taarifa rasmi inayolaani jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina na kusema kuwa, jinai hizo ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Cuba iliyotolewa leo mbali na kulaani jinai hizo za Israel imesisitiza kuwa, vitendo vinavyofanywa na Israel huko Palestina dhidi ya raia wasio na hatia yoyote ni ukiukaji wa wazi wa hati ya Umoja wa Mataifa na haki za binadamu.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba, vitendo vya kinyama vya wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza ni dhihirisho la wazi la kukanyaga na kukiuka haki za binadamu na kwamba, vitendo hivyo vinazidisha mizozo na mivutano katika eneo la Mashariki ya Kati.

Wapalestina wasiopungua 18 wameshauawa shahidi hadi sasa na wengine zaidi ya 1,900 wamejeruhiwa na askari wa utawala haramu wa Israel tangu yalipoanza maandamano ya siku ya ardhi yaliyopewa jina la  "Haki ya Kurejea" yaliyoanza huko Palestina siku ya Ijumaa.

Wapalestina wakiandamana kwa amani dhidi ya Israel

Katika siku ya kwanza ya maandamano hayo Wapalestina wasiongua 16 waliuawa kwa kupigwa risasi na askari wa utawala haramu wa Israel na wengine zaidi ya 1500 walijeruhiwa. Lengo la maandamano hayo ni kusisitiza haki ya wakimbizi wa Palestina ya kurejea katika ardhi zao zilizoghusubiwa na Israel. Maandamano hayo yanayofanyika kwa amani, yamekabiliwa kwa risasi za wanajeshi wa Israel.  

Mauaji yaliyofanywa na Israel dhidi ya raia wa Gaza ni kielelezo cha jinai za kivita kwa sababu raia hao wa Palestina wanalengwa kwa risasi bila ya kuwa na silaha ya aina yoyote.

Tags