Kikao cha G7 na hitilafu za ndani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i43566-kikao_cha_g7_na_hitilafu_za_ndani
Kikao cha siku mbili cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa G7 kimemaliza kazi zake huko Toronto nchini Canada.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 24, 2018 06:22 UTC
  • Kikao cha G7 na hitilafu za ndani

Kikao cha siku mbili cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa G7 kimemaliza kazi zake huko Toronto nchini Canada.

Kikao hicho kimejadili maudhui mbalimbali za kimataifa ikiwa ni pamoja na hali ya kiuchumi na kibiashara ya dunia ya sasa, uhusiano wa nchi za Magharibi na Russia, hali ya Syria, mazungumzo yajayo kati ya Marekani na Korea Kaskazini na mustakbali wa makubaliano ya nyuklia ya kundi la 5+1 na Iran. Kikao hicho cha Toronto pia kimefanya maandalizi ya mkutano ujao wa viongozi wa G7 uliopangwa kufanyika nchini Canada mwezi Juni mwaka huu. Mawaziri wa Mambo Nje wa G7 wamefanya jitihada za kujaribu kuondoa hitilafu zilizopo kati ya nchi wanachama katika kundi hilo.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa G7 wakiwa mkutanoni Toronto Canada na Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya, bi Federica Mogherini 

Kwa sasa maudhui kuu inayozusha hitilafu kubwa kati ya nchi zilizoendelea kiviwanda yaani G7 kwa kifupi ni masuala ya kiuchumi na sera za kibiashara za Rais Donald Trump wa Marekani. Tangu miezi kadhaa iliyopita Trump alitoa maagizo ya kuzidishwa ushuru wa forodha wa bidhaa zinazoagizwa kutoka baadhi ya nchi za kigeni. Sera hizo zinapingana na maslahi ya baadhi ya washirika wa kibiashara wa Marekani zikiwemo nchi nyingine sita wanachama katika G7. Hata hivyo ili kuepuka vita vya kibiashara na waitifaki wa serikali ya Washington, Donald Trump aliziondoa nchi za Canada, Japan na Umoja wa Ulaya katika orodha ya nchi zilizozidishiwa ushuru wa forodha. Pamoja na hayo vita vya kibiashara kati ya Marekani na China vitakuwa na taathira mbaya kwa ustawi wa kiuchumi wa nchi wanachama wa G7. Kwa msingi huo inaonekana kuwa, mkutano wa mwaka huu wa viongozi wa G7 utatawaliwa na kadhia ya biashara ya kimataifa na siasa za Trump katika uwanja huo.

Katika upande wa masuala ya kisiasa inaonekana kuna aina fulani ya mwafaka baina ya wanachama wa G7 kuhusu kadhia ya mustakbali wa uhusiano wa nchi za Magharibi na Russia na vilevile mazungumzo yajayo kati ya viongozi wa Marekani na Korea Kaskazini. Maudhui ya kupewa sumu jasusi wa zamani wa Russia nchini Uingereza, Sergei Skripal imeimarisha anga iliyo dhidi ya Russia kati ya pande mbili za Bahari ya Atlantic ingawa kupamba moto kwa hitilafu za nchi za Magharibi na Russia pai kumezusha wasiwasi baina ya pande hizo mbili.

Kiongozi wa chama cha mrengo wa kushoto nchini Ujerumani, Sahra Wagenknecht anasema: Kama kweli nchi za Maghaibi zinataka kufanya mazungumzo na Russia basi hazina budi kuialika Moscow katika kikao cha viongozi wa G7 kitakachofanyika nchini Canada.

Katika upande mwingine nchi za Ulaya na mwanachama pekee wa Asia katika G7 yaani Japan zimekaribisha sana mazungumzo yajayo kati ya Donald Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un. Hata hivyo Wajapani wana wasiwasi kwamba, yumkini katika mazungumzo hayo Marekani ikafikia makubaliano na Korea Kaskazini ambayo hayatatilia maanani maslahi ya Japan.

Rais Trump wa Marekani na Kiongozi wa Korea ya Kaskazini wanaotazamia kuwa na mazungumzo  katika siku zijazo 
 

Wakati huo huo maudhui ya makubaliano ya nyuklia na Iran maarufu kwa kifupi kwa jina la JCPOA yamezusha hitilafu kubwa zaidi baina ya Marekani na wanachama wengine wa G7 hususan wanachama wa Ulaya wa kundi hilo. Viongozi wa juu kabisa wa nchi hizo wamemtaka Rais wa Marekani aheshimu na kutekeleza majukumu ya nchi hiyo kuhusu makubliano ya nyuklia na Iran na kuacha kuhatarisha maslahi ya kimataifa. Kwa msingi huo inatupasa tusibiri na kuona kwamba, je, Donald Trump ataitikia wito na matakwa ya kimataifa zikiwemo nchi sita wanachama wa G7 ambao ni washirika wakubwa zaidi wa kiuchumi na kibiashara wa Marekani au la. Kitendawili hicho kitateguliwa tarehe 12 mwezi ujao wa Mei.