Vitendo vya unyanyasaji dhidi ya Waislamu vyaongezeka sana Austria
-
Polisi wa Austria wakiwatia mbaroni Waislamu
Kituo cha nyaraka na ushauri kuhusu masuala ya Waislamu nchini Austria kimetangaza habari ya kuongezeka sana vitendo vya unyanyasaji dhidi ya Waislamu barani Ulaya.
Shirika la habari la Anadolu limeripoti habari hiyo na kukinukuu kituo hicho kikisema kuwa, katika mwaka uliopita wa 2017 kulirikodiwa vitendo 309 vya kushambuliwa Waislamu nchini Austria ikiwa ni ongezeko la asilimia 21 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake yaani 2016.
Kituo hicho cha nyaraka na ushauri kuhusu masuala ya Waislamu cha Auistria kimeongeza kuwa, mkondo wa vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu nchini humo umekuwa ukipanda mwaka hadi mwaka huko Austria.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wanawake wa Kiislamu ndio wahanga wakuu wa unyanyasaji wa kijinsia katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kiasi kwamba wanaunda asilimia 98 ya Waislamu wanaoshambuliwa na watu wenye chuki za kidini na kunyanyaswa kijinsia katika nchi hiyo ya Ulaya.
Ni vyema tukasema hapa kwamba, mgogoro wa chuki dhidi ya Waislamu limekuwa ni tatizo kubwa kwa jamii za barani Ulaya katika miaka ya hivi karibu na kwamba vitendo vya unyanyasaji wa Waislamu vinazidi kuongezeka siku baada ya siku.