Ufaransa: Kuihifadhi JCPOA ni kipaumbele chetu, kujitoa ni kutangaza vita
https://parstoday.ir/sw/news/world-i44072-ufaransa_kuihifadhi_jcpoa_ni_kipaumbele_chetu_kujitoa_ni_kutangaza_vita
Mwakilishi wa kudumu wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, kuyalinda mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kwa jina la JCPOA ndicho kipaumbele cha nchi yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 05, 2018 03:23 UTC
  • Ufaransa: Kuihifadhi JCPOA ni kipaumbele chetu, kujitoa ni kutangaza vita

Mwakilishi wa kudumu wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, kuyalinda mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kwa jina la JCPOA ndicho kipaumbele cha nchi yake.

François Delattre amesema hayo alipohojiwa na shirika la habari la IRNA na kuongeza kuwa, mapatano ya nyuklia ya JCPOA ndiyo njia ya kuaminika ya kulinda usalama na amani duniani, na ndio maana Paris imelipa kipaumbele kikubwa suala la kulindwa mapatano hayo.

Kabla ya hapo Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alikuwa ameonya kuwa, iwapo Marekani itajitoa katika mapatano hayo, basi huenda hatua yake hiyo ikaitumbukiza dunia katika vita vipya.

Rais wa Marekani, Donald Trump ameyasaka mapatano ya JCPOA licha ya Washington kushiriki kikamilifu kufanikisha mapatano hayo ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1

 

Akihojiwa na gazeti la Der Spiegel, Macron amegusia vitisho vinavyotolewa na rais wa Marekani, Donald Trump vya kujitoa kwenye mapatano hayo na kusema, kitendo hicho kitakuwa ni sawa na kufungua "boksi la madudu" na kuisukuma dunia katika vita.

"Sidhani kama Donald Trump anapenda kutokee vita," amesema rais huyo wa Ufaransa.

Aidha amesema: "Kwa mtazamo wangu - ingawa sijui rais wenu ataamua nini - lakini nahisi kwamba atajitoa katika mapatano hayo kwa sababu zake mwenyewe zinazohusiana na masuala ya ndani ya Marekani." Aidha amesisitiza kuwa, hatua hiyo inaweza kumsaidia Trump kwa muda mfupi, lakini ni upuuzi katika malengo ya muda wa wastani na ya muda mrefu.

Tangu katikati ya mwezi Januari mwaka huu wakati aliporefusha vikwazo vipya dhidi ya Iran, Trump alitishia kuwa atajitoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA iwapo hayatafanyiwa marekebisho anayoyataka.