Marekani kuziuzia Saudia na Imarati 'mabomu-erevu' 120,000
https://parstoday.ir/sw/news/world-i44868-marekani_kuziuzia_saudia_na_imarati_'mabomu_erevu'_120_000
Rais Donald Trump ameliomba Bunge la Kongresi la Marekani litathmini mpango wa kuziuzia Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu makumi ya maelfu ya mabomu-erevu ya kuelekezwa, licha ya makelele ya jamii ya kimataifa ya kupinga utumiaji silaha hizo dhidi ya wananchi wa Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 23, 2018 02:56 UTC
  • Marekani kuziuzia Saudia na Imarati 'mabomu-erevu' 120,000

Rais Donald Trump ameliomba Bunge la Kongresi la Marekani litathmini mpango wa kuziuzia Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu makumi ya maelfu ya mabomu-erevu ya kuelekezwa, licha ya makelele ya jamii ya kimataifa ya kupinga utumiaji silaha hizo dhidi ya wananchi wa Yemen.

Trump ameliambia bunge hilo kuwa, hatua ya kuziuzia Saudia na Imarati silaha hizo zipatazo 120,000  mbali na kuipa Marekani mabilioni ya dola, pia itatoa nafasi nyingi za ajira kwa Wamarekani.

Mwezi Novemba mwaka jana, Riyadh ilikubali kununua silaha hizo za kisasa kwa thamani ya dola bilioni 7 za Marekani, kutoka mashirika ya kuunda silaha ya Marekani.

Saudia na washirika wake wamekuwa wakitumia silaha hizo zikiwemo zilizopigwa marufuku kimataifa katika hujuma zake dhidi ya Wayemen.

Sehemu ya hujuma za anga za Saudia dhidi ya Yemen

Saudia ilitumia mabomu haramu ya vishada katika shambulizi la tarehe 10 ya mwezi huu katika eneo la Hamadan katika mkoa wa Sana'a, ambapo kwa akali watu sita wakiwemo watoto wawili waliuawa.

Ikumbukwe kuwa Saudia ilianzisha mashambulizi yake dhidi ya Yemen mnamo Machi mwaka 2015 kwa lengo la kuirejesha madarakani serikali kibaraka ya Abdu Rabuh Mansour Hadi, aliyejiuzulu urais na kukimbilia Riyadh, ambapo watu zaidi ya 14,000 wameuawa na mamilioni ya wengine kujeruhiwa.