Jun 22, 2018 04:52 UTC
  • EuroMed Rights: Ukatili dhidi ya wahajiri unaongezeka barani Ulaya

Shirika la kutetea haki za binadamu Ulaya na Mediterania, (EuroMed Rights) limetahadharisha kuhusu ongezeko la ukatili na vitendo vya kutumia mabavu dhidi ya wahajiri katika nchi za Ulaya na limeutaka Umoja wa Ulaya (EU) kukabiliana na ubaguzi barani humo.

Ripoti iliyotolewa na EuroMed Rights imeutaka Umoja wa Ulaya kukabiliana na miito inayochochea chuki na ubaguzi dhidi ya wahajiri na wakimbizi na kuchukua msimamo imara wa kukabiliana na sera za kuwapiga vita raia wa kigeni na ukiukaji wa haki za wakimbizi na wahajiri ambavyo ni matokeo ya siasa za makundi yenye misimamo ya kufurutu mipaka ya mrengo wa kulia barani Ulaya.

Kituo hicho cha kutetea haki za binadamu chenye makao yake mjini Geneva kimesisitiza kuwa, mbinu za kueneza chuki dhidi ya raia wa kigeni na ubaguzi dhidi ya wahajiri na wakimbizi ni pamoja na manyanyaso ya kimwili, kuchomwa moto kwa makusudi, mauaji, kuwazuia wakimbizi na wahajiri kutoka nje ya kambi zao, kuzuia mishahara ya wahajiri au kuwazuia kueleza utambulisho wao wa kidini kama vile vazi la hijabu la mwanamke wa Kiislamu. 

Ripoti iliyotolewa mwaka jana ilionesha kuwa, kulifanyika zaidi ya mashambulizi elfu moja dhidi ya Waislamu na milki zao katika nchi za Ulaya. 

EuroMed Rights imetoa wito wa kufanyika jitihada kubwa zaidi za kulinda haki za wakimbizi na wahajiri katika nchi za bara hilo kwa mujibu wa sheria na makubaliano ya kimataifa. 

Tags