Seneti ya Uholanzi yapiga marufuku vazi la burqa
(last modified Tue, 26 Jun 2018 15:51:55 GMT )
Jun 26, 2018 15:51 UTC
  • Seneti ya Uholanzi yapiga marufuku vazi la burqa

Bunge la Seneti la Uholanzi limepasisha muswada wa sheria inayopiga marufuku vazi la stara la burqa linalovaliwa na baadhi ya wanawake Waislamu nchini humo.

Muswada huo ambao ulipasishwa mwishoni mwa mwaka 2016 na Bunge la Chini la Uholanzi, unapiga marufuku kuvaa burqa katika majengo ya serikali, vituo na vyombo vya usafiri wa umma, katika mashule na hospitali.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, yeyote atakayevaa vazi hilo la stara katika maeneo yaliyotajwa atatozwa faini ya Euro 405 sawa na dola 430 za Marekani.

Haya yanajiri chini ya wiki mbili, baada ya Geert Wilders, kiongozi wa chama chenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia nchini humo kupewa kibali cha kuandaa mashindano ya kuwasilisha vibonzo vya kumvunjia heshimu Mtume Muhammad SAW.

Vazi la burqa

Februari mwaka huu na katika kuendeleza vitendo vya unyanyasaji na chuki dhidi ya Waislamu, watu wenye chuki za kidini waliuchoma moto msikiti mmoja katika mji wa Drachten wa kaskazini mwa Uholanzi.

Oktoba mwaka 2016, Bulgaria ilijiunga na baadhi ya nchi za Magharibi zilizopiga marufuku vazi la burqa kama vile Canada, Ubelgiji na Ufaransa, baada ya bunge la nchi hiyo kupasisha sheria inayopiga marufuku vazi hilo linalovaliwa na baadhi ya wanawake Waislamu nchini humo.

 

Tags