Ripoti: Kiwango cha chuki dhidi ya Uislamu Uingereza kimevunja rekodi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i46945-ripoti_kiwango_cha_chuki_dhidi_ya_uislamu_uingereza_kimevunja_rekodi
Ripoti mpya ya asasi isiyokuwa ya kiserikali imesema uhalifu unaotokana na chuki dhidi ya Waislamu na matukufu yao umeongezeka kwa kiwango cha kutia wasiwasi nchini Uingereza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 22, 2018 09:38 UTC
  • Ripoti: Kiwango cha chuki dhidi ya Uislamu Uingereza kimevunja rekodi

Ripoti mpya ya asasi isiyokuwa ya kiserikali imesema uhalifu unaotokana na chuki dhidi ya Waislamu na matukufu yao umeongezeka kwa kiwango cha kutia wasiwasi nchini Uingereza.

Shirika hilo linaloitwa Tell Mama limesema katika ripoti yake ya kila mwaka kwamba, kati ya kesi 1,201 za hujuma hizo zilizonakiliwa na kufanyiwa uhakiki mwaka jana 2017, kumedhihirisha kuwa kiwango cha chuki hizo kimeongezeka kwa asilimia 26 ikilinganishwa na mwaka juzi wa 2016. Kiwango hicho ndicho cha juu zaidi tangu shirika hilo lianze kunakili visa vya kuhujumiwa Waislamu, taasisi na maeneo yao ya ibada nchini Uingereza.

Ripoti ya shirika hilo lenye makao yake mjini London imefichua kuwa, watu sita kati ya kumi waliohujumiwa ni wanawake, na kwamba watekelezaji wa jinai hizo wanane kati ya kumi ni wanaume hususan wenye umri kati ya miaka 13 na 18.

Iman Atta, Mkurugenzi wa Tell Mama amesema "Tuna wasiwasi mkubwa sana na kuongezeka kiwango cha uhalifu unaotokana na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu Uingereza, na mbaya zaidi, hujuma hizo hufanywa zaidi na tabaka la vijana."

Waislamu wakiandamana kupinga chuki dhidi ya Uislamu

Mwezi uliopita, zaidi ya misikiti 350 na jumuiya za Kiislamu nchini Uingereza zilitaka uchunguzi ufanyike kuhusu chuki dhidi ya Uislamu miongoni mwa wanachama wa ngazi za juu wa chama tawala cha Conservative.

Kwa mujibu wa sensa ya hivi karibuni ya watu Uingereza, kuna Waislamu milioni 2.8 kati ya watu milioni 64 nchini humo.