Madai ya Donald Trump ya kuwa tayari kufikia makubaliano na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i47006-madai_ya_donald_trump_ya_kuwa_tayari_kufikia_makubaliano_na_iran
Licha ya kuweko uadui na uhasama wa Marekani dhidi ya Iran katika kipindi cha miaka takribani 40 tangu kuasisiwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, lakini katika kipindi cha uongozi wa Rais Donald Trump, uadui huo ulishadidi zaidi iwe ni katika kipindi cha kampeni za uchaguzi na hata baada ya kuingia madarakani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 25, 2018 03:48 UTC
  • Madai ya Donald Trump ya kuwa tayari kufikia makubaliano na Iran

Licha ya kuweko uadui na uhasama wa Marekani dhidi ya Iran katika kipindi cha miaka takribani 40 tangu kuasisiwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, lakini katika kipindi cha uongozi wa Rais Donald Trump, uadui huo ulishadidi zaidi iwe ni katika kipindi cha kampeni za uchaguzi na hata baada ya kuingia madarakani.

Trump ameyabeza na kuyaponda mara chungu nzima makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) na kuyataja kuwa makubaliano mabaya zaidi kwa Marekani. Ni kwa msingi huo ndio maana Mei 8 mwaka huu, Trump akatangaza kuiondoa nchi yake katika makubaliano hayo. Kwa mtazamo wa Trump ni kuwa, JCPOA yalikuwa ni maafa kwa Marekani. Katika siku za hivi karibuni mjadala mkali wa kurushiana maneno kati ya Iran na Marekani umeshadidi.

Jumapili iliyopita Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa hotuba kali akijibu vitisho vya Trump aliyesema kwamba hataruhusu mafuta ya Iran kuuzwa nje ya nchi na kusema: Iran imekuwa ikilinda njia za baharini za Mashariki ya Kati katika kipindi chote cha historia, hivyo usicheze na mkia wa simba, utajuta kwa sababu jibu la Iran litakuwa kali sana." 

Rais Hassan Rouhani wa Iran

Akijibu matamshi ya Rais Hassan Rouhani wa Iran aliyeitaka Marekani "isichezee mkia wa simba", juzi Donald Trump aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Ukitoa tena vitisho dhidi ya Marekani, Iran itashuhudia matokeo mabaya ambayo yameshuhudiwa mara chache sana katika historia."

Pamoja na hayo na licha ya bwabwaja na bwata zake za hivi karibuni, Trump ameibuka na kudai kwamba, Marekani iko tayari kufikia makubaliano na Iran. Akihutubia jana katika mji wa Kansas mbele ya hadhara ya maveterani wa vita Trump alisema: Tuko tayari kufikia makubaliano ya kweli na Iran. 

Swali linaloulizwa na wengi ni hili kwamba, Trump anazungumzia utayarifu wa kufikia makubaliano gani na Iran? kwa kuzingatia misimamo na matakwa ya serikali ya Marekani kwa Iran ambaye yazingumziwa katika fremu ya matakwa 12 ya Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya kigeni wa Marekani tunaweza kusema kuwa, kwa mtazamo wa Washington ni kuwa, itafikia makubaliano na Iran pale taifa hili litakapokuwa tayari kuyakubali matakwa yote ya Marekani kibubusa na bila ya kuhoji chochote. Kwa msingi huo basi, huko si kufikia makubaliano kati ya pande mbili bali ni upande mmoja kusalimu amri kikamilifu mbele ya upande wa pili. 

Wendy Sherman, Naibu Waziri wa zamani wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani

Labda ndio maana hata tangazo la matakwa ya Marekani likafanyiwa masihara na dhihaka na wakosoaji wa Trump ndani na nje ya nchi hiyo. Wendy Sherman, aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amemfananisha Trump na mtoto mdogo wa shule na kusema: Tunamuona mtoto mdogo wa kiume wa shule anajitutumua  na kuonyesha kwamba, ana nguvu, katika hali ambayo kile ambacho tunakabiliwa nacho ni udhaifu na kutokuweko usalama. Wairani hawasalimu amri. 

Bila shaka matamshi hayo ya Sherman ni kuashiria mwenendo Iran wa kutosalimu amri na kupinga dhulma katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita na kusimama kwake kidete mbele ya aina kwa aina ya njama za siri na za dhahiri za Marekani. Hivi sasa Trump anadhani kwamba, kwa kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi ambavyo havijawahi kushuhudiwa ataifanya nchi hii isalimu amri.

Donald Trump akitumia vikwazo kama wenzo wa kufikia malengo yake anajaribu kadiri inavyowezekana kuyafanya maisha ya wananchi kuwa magumu na yasiyostahamilika, ili kwa njia hiyo kama anavyodai mwenyewe aandae mazingira ya kutokea vurugu na machafuko ya ndani. Hatua hizo za Marekani bila shaka ni kuingilia masuala ya ndani ya Iran, jambo ambalo linakinzana bayana na sheria za kimataifa na ni kinyume kabisa na misingi ya kimataifa na hati ya Umoja wa Mataifa.

Waandamanaji nchini Iran wakichoma moto bendera za Marekani na Israel

Utendaji wa Trump kuhusiana na Iran unaweka wazi ukweli huu kwamba, kiongozi huyo mwenye kuropoka ovyo bado hajawafahamu Wairani. 

Tajiriba ya miaka 40 iliyopita inaonyesha kuwa, kadiri mashinikizo kutoka nje dhidi ya Iran yalivyoongezeka, ndivyo ambavyo pia mshikamano na mfungamano wa ndani nchini Iran ulivyoimarika zaidi. Duru mpya ya hatua zilizo dhidi ya Iran inafanyika katika hali ambayo, kinyume na huko nyuma, hivi sasa Washington imebaki peke yake. 

Kwa kuzingatia kufungamana kikamilifu Iran na makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili ya Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), mataifa mengine hususan nchi wanachama wa kundi la 4+1, hazioni sababu ya kuwa pamoja na Marekani katika kuiwekea tena vikwazo Tehran. Kimsingi ni kuwa, ulimwengu umesimama katika safu moja na unapinga hatua za Trump dhidi ya taifa la Iran.