Sep 19, 2018 14:31 UTC
  • Hillary Clinton awataka wananchi wa Marekani wakabiliane na siasa za udikteta za Donald Trump

Hillary Clinton, Waziri wa zamani wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani ametahadharisha kwamba, endapo Rais wa sasa wa nchi hiyo Donald Trump ataachwa afanye atakacho na kutokuweko uangalizi na usimamizi juu yake, basi nchi hiyo ijiandae kukabiliwa na matokeo hasi na mabaya.

Hillary Clinton ambaye alichuana na Donald Trump katika kinyang’anyiro cha urais nchini Marekani mwaka 2016 akipeperusha bendera ya chama cha Democrat na kushindwa, amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na Kanali ya Televisheni ya MSNBC na kuwataka wananchi wa Marekani wakabiliane na kile alichokiita “mielekeo ya kidikteta” ya Rais Donald Trump.

Bi Clinton amesema kuwa, endapo wananchi wa Marekani wataupuuza uchaguzi mdogo ujao wa Marekani, basi kutashuhudiwa uharibifu na maangamizi ya asasi muhimu za Marekani hatua ambayo itakuwa na matokeo mabaya mno.

Rais Donald Trump wa Marekani 

Waziri huyo wa zamani wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani ambaye amekuwa akimkosoa vikali Trump amewahi kunukuliwa pia akisema kwamba, hatua ya Rais Donald Trump ya kuvuruga mapatano ya nyuklia ya Iran ya mwaka 2015 ni jambo ambalo limeifanya Marekani ionekane kuwa nchi duni na ya kijinga.

Sambamba na kukaribia uchaguzi mdogo wa Marekani utakaofanyika mwaka huu, hivi sasa kunashuhudiwa kushadidi malumbano na misimamo hasi dhidi ya kila upande baina ya vyama viwili vikuu vya siasa nchini Marekani vya Republican na Democrat.

Uchaguzi huo mdogo wa Marekani ambao unatarajiwa kuchagua wawakilishi 435 wa Bunge na thuluthi moja ya wawakilishi wa Bunge la Seneti umepangwa kufanyika tarehe 6 Novemba mwaka huu.

Tags