Erdogan: Mauaji ya Khashoggi yalipangwa, wahusika washtakiwe Istanbul
Rais Recep Tayyib Erdogan wa Uturuki amesema watu wote waliohusika na mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari na mkosoaji mkubwa wa utawala wa Saudi Arabia wanapashwa kubebeshwa dhima na kesi zao zinapaswa kusikilizwa mjini Istanbul.
Akihutubia wabunge wa chama tawala katika Bunge la nchi hii leo, Erdogan amesema kuna haja watu 18 wanaoshukiwa kuhusika na mauaji ya Khashoggi wawajibishwe kisheria katika mahakama ya mji wa Istanbul ambako mkosoaji huyo wa utawala wa Aal-Saud aliuawa.
Amesema mauaji hayo yalipangwa siku nyingi kabla ya kutekelezwa, na kwamba kulikuwepo na ramani ya njia ya kufuatwa katika utekelezaji wake.
Rais wa Uturuki amehoji, "kwa nini raia hao 15 wa Saudia walikutana Istanbul? Nani aliwapa maagizo hayo? Kwa nini ubalozi mdogo wa Istanbul haukufunguliwa mara moja baada ya kuuawa Khashoggi bali siku kadhaa baadaye?
Huku akizungumza kwa ghadhabu na hamaki, Rais wa Uturuki amesema kwa nini Saudia hadi sasa haijaukabidhi mwili wa Khashoggi licha ya kukiri kuwa aliuawa katika ubalozi huo mdogo wa Istanabul?
Kadhalika ameutaka utawala wa Aal-Saud kumfichua raia wa Uturuki ambaye Riyadh inadai ilimkabidhi mwili wa Khashoggi baada ya kuuawa.
Amesema ni kwa nini hifadhi ya matukio yaliyorekodiwa na kamera za usalama za CCTV katika ubalozi huo wa Istanbul ilifutwa iwapo mauaji hayo hayakufanyika kwa mpangilio maalumu?
Sanjari na kutoa mwito wa kuundwa Kamisheni Huru ya Uchunguzi, Rais Erdogan amesema mauaji hayo yamekiuka Muafaka wa Vienna unaowapa kinga ya kidiplomasia raia wanapokuwa katika ofisi zao za kibalozi.