Utafiti: Ubaguzi wa rangi umeongezeka duniani
Taasisi kwa ajili ya Uchumi na Amani (IEP) imeeleza katika ripoti yake mpya kuwa, idadi ya waathirika wa vitendo vya ubaguzi wa rangi iliongezeka na takwimu za watu waliouawa kutokana na mashambulio ya kigaidi ilipungua katika mwaka uliopita wa 2017.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi hiyo ya Institute for Economic and Peace yenye makao yake mjini Sydney, Australia, vielezo vya kimataifa kuhusu ugaidi katika mwaka 2018 vinaonyesha kuwa, maafa ya roho za watu yaliyotokana na mashambulio ya kigaidi katika mwaka 2017 yalipungua kwa asilimia 27, lakini kundi la kigaidi la DAESH (ISIS) lingali ni kundi hatari zaidi la kigaidi duniani.
Katika mwaka huo uliopita, nchi 67 zilishuhudia kwa akali kesi moja ya mtu aliyeuawa kutokana na shambulio la kigaidi ambacho ni kiwango cha chini kulinganisha na mwaka 2016; wakati katika mwaka 2016 nchi 79 ziliripoti tukio lisilopungua moja la kifo kilichotokana na hujuma ya kigaidi.
Sehemu nyingine ya ripoti ya IEP imeeleza kuwa: Afghanistan, Nigeria, Somalia, Pakistan, Misri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati na India ni miongoni mwa nchi zilizoripoti idadi kubwa zaidi ya vifo vilivyosababishwa na mashambulio ya kigaidi.
Ripoti ya Taasisi kwa ajili ya Uchumi na Amani imebainisha pia kuwa watu 17 waliuawa katika jumla ya hujuma na mashambulio 31 yaliyofanywa na makundi ya mrengo wa kulia yenye misimo mikali na chuki za ubaguzi wa rangi, ambapo mengi ya mashambulio hayo yalifanywa na mtu mmoja mmoja dhidi ya Waislamu.
Kwa mujibu wa IEP, jinai na uhalifu uliofanywa na makundi hayo ya mrengo wa kulia yenye misimamo ya kufurutu mpaka viliongezeka katika nchi za Marekani na Canada, ambapo mnamo mwezi uliopita wa Novemba, Polisi ya Upelelezi ya Marekani FBI ilitangaza kuwa uhalifu uliofanywa kutokana na chuki umeongezeka kwa asilimia 17 mwaka huu kulinganisha na 2017, wakati nchini Canada ongezeko hilo ni la karibu asilimia 50.../