Marekani imewatenganisha makumi ya watoto wa wahajiri na familia zao
https://parstoday.ir/sw/news/world-i49997-marekani_imewatenganisha_makumi_ya_watoto_wa_wahajiri_na_familia_zao
Shirika la habari la Associated Press limevujisha data za serikali ya Washington zinazoonesha kuwa, Marekani imewatenganisha makumi ya watoto wa wahajiri na familia zao katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico ndani ya miezi michache iliyopita.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Dec 06, 2018 11:20 UTC
  • Marekani imewatenganisha makumi ya watoto wa wahajiri na familia zao

Shirika la habari la Associated Press limevujisha data za serikali ya Washington zinazoonesha kuwa, Marekani imewatenganisha makumi ya watoto wa wahajiri na familia zao katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico ndani ya miezi michache iliyopita.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto wasiopungua 81 wametenganishwa na wazazi na watu wengine wa familia zao katika mpaka huo tokeo mwezi Juni mwaka huu hadi sasa.

Ripoti hiyo ya Associated Press imefichua kuwa, katika msimu wa joto kali, watoto zaidi ya 2,400 wa wahajiri walitenganishwa na wazazi wao nchini Marekani, huku vyombo vya usalama vya nchi hiyo vikiwazuilia wazazi na watu wengine wa familia za watoto hao.

Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International (AI) lilisema kuwa, hatua iliyochukuliwa na serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuwatenganisha watoto wadogo na wazazi wao wahajiri ni miongoni mwa jinai mbaya zaidi zilizowahi kushuhudiwa duniani.

Rais Donald Trump wa US

Kadhalika Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema hatua ya serikali ya Marekani ya kuwatenganisha watoto wa wahajiri na wazazi wao katika mpaka wa Mexico ni ya kikatili na haikubaliki.

Serikali ya Trump kuanzia katikati ya mwezi Aprili hadi katikati ya mwezi Juni pekee mwaka huu, iliwatenganisha maelfu ya watoto na wazazi wao ambao walitiwa nguvuni kwa tuhuma za kuingia katika ardhi ya Marekani kinyume na sheria.