Umoja wa Mataifa: Waislamu 15,000 Warohingya wamekimbia Myanmar hivi karibuni
Nyaraka zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, Waislamu 15,000 wa jamii ya Rohingya wamekimbia kutoka Myanmar katika siku za hivi karibuni.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa, mwenendo wa Waislamu hao wa jimbo la Rakhine kukimbilia nchini Bangladesh unaendelea kutokana na kuzidi kuandamwa na maudhi na mateso na hata mauaji.
Yanghee Lee, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Mynamar ametangaza kuwa, inaonekana serikali ya Myanmar haina uamuzi wa kweli wa kurejea nchini humo mamia ya maelfu ya Waislamu Warohingya waliolazimika kukimbilia katika nchi jirani ya Bangladesh, kwani takwimu mpya zinaonyesha kuwa, Waislamu 15,000 wa jimbo la Rakhine wameikimbia nchi hiyo hivi karibuni.
Ripota huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Myanmar ameeleza kuwa, vijiji na nyumba nyingi za Waislamu wa Rohingya katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa nchi hiyo zimeteketezwa kabisa na kusawazishwa na ardhi.
Maelfu ya Waislamu wameuawa na wengine karibu milioni moja wamelazimishwa kuwa wakimbizi nchini Myanmar kutokana na mashambulizi yanayoendelea kufanywa na jeshi la nchi hiyo likishirikiana na Mabudha wenye misimamo mikali.
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, jeshi la Myanmar limefanya mauaji ya kimbari dhidi ya jamii wa Waislamu wa nchi hiyo hususan katika jimbo la Rakhine.