Amnesty yaitaka Marekani isitishe ukatili dhidi ya wahajiri
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limekosoa sera za kikatili za serikali ya Marekani kuhusiana na wahajiri na kutoa wito wa kubadilishwa mwenendo huo.
Taarifa ya Amnesty International imetolewa baada ya kufariki dunia mtoto mwingine mhajiri katika mahabusu ya Marekani iliyoko kwenye mpaka wa nchi hiyo na Mexico. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, serikali ya Marekani inalazimika kukomesha sera zake zilizodhidi ya wahajiri na kuzuia maafa zaidi kwa watoto wao.
Siku chache baada ya kufariki dunia Jakelin Caal Maquin, binti aliyekuwa na umri wa miaka saba mhajiri kutoka Guatemala aliyekuwa akishikiliwa kizuizini nchini Marekani, Idara ya Wakala wa Forodha na Hifadhi ya Mipaka ya nchi hiyo imetangaza habari ya kufariki dunia mtoto mwingine mhajiri aliyekuwa na umri wa miaka 8 katika kizuizi cha wakala huo.
Wanasheria na makundi ya kutetea haki za binadamu yameukosoa vikali Wakala wa Mipaka na Forodha wa Marekani kutokana kifo cha mtoto huyo wa pili mhajiri akiwa katika kizuizi chake.
Baada ya kufariki dunia watoto hao wahajiri mikononi mwa maafisa wa serikali ya Marekani, sasa Idara ya Forodha na Hifadhi ya Mipaka ya Marekani ambayo iko chini ya mashinikizo makubwa ya ndani na nje ya nchi, imetoa amri ya kufanyiwa uchunguzi wa kitiba watoto wote wanaoshikiliwa katika vizuizi vya nchi hiyo.
mapema wiki hii Umoja wa Mataifa ulitoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusiana na kifo cha Jakelin Caal Maquin, binti aliyekuwa na umri wa miaka saba mhajiri wa Guatemala aliyefia kizuizini nchini Marekani.