Carter: Dunia inakabilwia na hatari ya "Vita Baridi vya Kisasa"
https://parstoday.ir/sw/news/world-i50570-carter_dunia_inakabilwia_na_hatari_ya_vita_baridi_vya_kisasa
Rais wa zamani wa Marekani amesema kuwa nchi hiyo inaingia tena katika Vita Baridi lakini mara hii ni dhidi ya China.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 01, 2019 23:19 UTC
  • Carter: Dunia inakabilwia na hatari ya

Rais wa zamani wa Marekani amesema kuwa nchi hiyo inaingia tena katika Vita Baridi lakini mara hii ni dhidi ya China.

Jimmy Carter ambaye alikuwa akizungumza kwa mnasaba wa kutimia mwaka wa 40 wa kurejeshwa na kuboreshwa uhusiano wa Marekani na China, ameeleza wasiwasi wake kuhusiana na matamshi yanayotolewa na maafisa wa nchi hizo mbili na kusema iwapo matamshi hayo yatathibitishwa itakuwa vigumu kusimamisha Vita Baridi vya Kisasa baina ya pande hizo mbili. 

Carter amesema kuwa, katika kipindi nyeti cha sasa, suitafahamu, mahesabu yasiyo sahihi na kutofuata sheria kuhusu maeneo kama ya Taiwan na Bahari ya China vinaweza kusababisha mizozo na hata vita na mapigano ya silaha na wakati huo kutatokea maafa makubwa duniani. 

Jimmy Carter: Kuna uwezekano wa kutokea vita baina ya Marekani na China.

Rais wa zamani wa Marekani amesema kuwa, njia nyepesi zaidi ya ushirikiano wa Marekani na China ni kanda ya Afrika na kwamba nchi hizi mbili zinaweza kutumia ushirikiano katika eneo hilo kwa ajili ya kuondoa hali ya kutoaminiana na kuanzisha uhusiano mzuri zaidi. 

Mwanzoni mwa mwaka uliomalizika wa 2018 Rais Donald Trump wa Marekani alianzisha vita vya kiuchumi na kibiashara dhidi ya nchi kadhaa ikiwemo China kwa kuzidisha ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazoingizwa Marekani kutoka katika nchi hizo. Hatua hiyo ilipingwa vikali kimataifa na kukabiliwa na jibu mfano wake kutoka China.