Mapinduzi ya kisiasa ya Marekani dhidi ya Rais Maduro wa Venezuela
Tangu kuingia madarakani nchini Venezuela serikali ya mrengo wa kushoto hapo mwaka 1999 hadi sasa, Marekani daima imekuwa ikifanya juhudi za kudhoofisha na kuingo'a mamlakani serikali hiyo.
Serikali ya Washington si tu kwamba imekuwa ikiuwanga mkono waziwazi wapinzani wa serikali ya Caracas bali imekuwa ikishirikiana kwa karibu na washirika wake katika eneo la Amerika ya Latini kwa madhumuni ya kukabiliana na Rais Nicolás Maduro wa Venezuela ambapo imekuwa ikitoa mashinikizo ya kumtaka ajiuzulu au impindue kijeshi. Akizungumza hivi karibuni mbele ya waandishi habari huko Caracas, mji mkuu wa Venezuela, Rais Maduro alisema kwamba John Bolton, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani ndiye anayeongoza mipango na njama za kuzusha ghasia na machafuko nchini Venezuela kwa lengo la kuipindua serikali ya nchi hiyo. Baada ya Juan Guaido, spika aliyeondolewa madarakani wa bunge la taifa la Venezuela kutangaza na kujiapisha kuwa rais wa nchi hiyo, Rais Donald Trump wa Marekani alitoa taarifa akitangaza kumtambua rasmi mwanasiasa huyo kuwa rais wa muda wa Venezuela, hatua ambayo imechukuliwa kuwa mapinduzi ya kisiasa dhidi ya rais halali wa nchi hiyo.
Lengo la hatua hiyo ya Trump ni kuandaa uwanja wa kuipindua kijeshi serikali halali iliyochaguliwa kidemokrasia na wananchi wa Venezuela. Licha ya kudai kuwa hana nia ya kuipindia kijeshi serikali hiyo, lakini Trump ameendelea kusisitiza kuwa machaguo yote yako mezani. Katika kuifuata kibubusa Marekani, nchi kadhaa za Amerika ya Latini zikiwemo Chile, Peru, Colombia, Parague, Brazil na Argentina zimetangaza kumtambua rasmi Guaido kuwa rais wa muda wa Venezuela. Huku akimtuhumu Rais Maduro kuwa dikteta, Mike Pence, Makamu wa Rais wa Marekani alisema waziwazi siku ya Jumanne kwamba nchi hiyo inaunga mkono kila aina ya machafuko na ghasia zinazolenga kuipindua serikali ya sasa ya Venezuela. Wakati huohuo Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ameingilia waziwazi mambo ya ndani ya Venezuela kwa kuwachochea wapinzani dhidi ya serikali halali ya nchi hiyo. Kuhusu hilo, Joe McMonigle, mtaalamu wa masuala ya nishati anasema kwamba kuna watu katika White House ambao wanataka hatua muhimu zichukuliwe dhidi ya Venezuela. Iwapo wataamua kuchukua hatua, ni wazi kuwa watachukua hatua ambazo ni kali mno.
Uchochezi huo wa Marekani umekabiliwa a radiamali kali ya Rais Maduro ambaye amesisitiza kwamba hatasalimu amri mbele ya vitisho na uchochezi huo wa Marekani. Akizungumza na umati mkubwa wa wafuasi wake mbele ya ikulu ya nchi hiyo, Rais Maduro ametangaza kukata uhusiano wa kidiplomasia na Marekani na wakati huohuo kuwapa wanadiplomasia wa nchi hiyo masaa 72 waondoke katika ardhi ya nchi hiyo. Katika kujibu makataa hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amedai kwamba Maduro hana tena mamlaka ya kuwaamrisha wanadiplomasia wa Marekani waondoke Venezuela na kwamba amri hiyo haitambuliwi rasmi na watawala wa Marekani. Maduro amekuwa akiashiria mara kwa mara nafasi hasi na haribifu ya Marekani katika masuala ya ndani ya Venezuela. Licha ya kuwepo uungaji mkono wa baadhi ya nchi za Marekani ya Latini kwa hatua hizo za kichochezi za Marekani dhidi ya Venezuela, lakini nchi kama vile, Bolivia, Cuba, Mexico, Russia na Uturuki zimetangaza wazi uungaji mkono wao kwa Rais Maduro wa nchi hiyo. Katika uchaguzi mkuu wa rais uliofanyika mwezi Mei mwaka uliopita, Maduro alipata karibu asilimia 68 ya kura zilizopigwa na hivyo kufanikiwa kuhudumia kipindi cha pili cha urais wake.
Licha ya hayo, kuna uwezekano mkubwa wa Venezuela kushuhudia machafuko makubwa katika siku zijazo, kwa kutilia maanani hatua ya Guaido ya kujitangaza kuwa rais wa muda wa nchi hiyo na vilevile fitina kubwa inayofanywa na Marekani nchini humo kwa ajili ya kuwachochea wananchi wa nchi hiyo wasimame dhidi ya serikali ya Maduro. Wakati huohuo, Marekani sasa imepata fursa nzuri ya kutekeleza mashambulio ya kijeshi dhidi ya serikali ya Venezuela, kupitia uungaji mkono wa Guaido, kibaraka wa Marekani aliyejitangaza kuwa rais wa muda wa nchi hiyo.