Ripoti: Kiwango cha ufisadi kimekithiri Marekani katika utawala wa Trump
Ripoti ya shirika la kutathmini viwango vya ufisadi duniani la Transparency International imesema kiwango cha ufisadi na visa vya rushwa vimeogezeka pakubwa nchini Marekani tangu Rais Donald Trump aingie madarakani.
Katika ripoti yake ya kila mwaka, shirika hilo lenye makao yake mjini Berlin nchini Ujerumani limesema kuwa, Marekani imepoteza alama nne na kuambulia alama 71 kati ya 100, katika Viwango vya Ufisadi kwa mwaka uliopita 2018.
Transparency International amesema kiwango cha ufisadi nchini Marekani kimeongezeka kwa kiasi kikubwa ambacho hakijawahi kushuhudiwa tokeo mwaka 2011.
Ripoti ya shirika hilo la kutathmini viwango vya ufisadi duniani imesema mmomonyoko wa maadili umekithiri mno katika taasisi za Marekani hususan katika ngazi za juu.
Rais Trump amekuwa akiandamwa na malalamiko na ukosoaji mkubwa kwa kuwapa nafasi za juu serikalini watu wa karibu wa familia yake, tangu aingie usukani Januari mwaka 2017.
Shirika la Transparency International limesema Denmark na New Zealand ndizo nchi zenye viwango vya chini vya ufisadi, huku Somalia, Yemen na Sudan Kusini zikitajwa kuongoza katika viwango vya ufisadi duniani.