Jeshi la Venezuela latangaza tena utiifu wake kwa Rais Maduro
(last modified Thu, 21 Feb 2019 02:55:59 GMT )
Feb 21, 2019 02:55 UTC
  • Jeshi la Venezuela latangaza tena utiifu wake kwa Rais Maduro

Waziri wa Ulinzi wa Venezuela ametangaza tena utiifu wake na vikosi vya majeshi ya nchi hiyo kwa Rais Nicolas Maduro wa nchi hiyo na kusema kuwa, makamanda na wanajeshi wa nchi hiyo wanafuata na kuutii amri ya Rais Maduro na wataendelea kusimama naye bega kwa bega hadi tone la mwisho la damu yao.

Vladimir Padrino López ameyasema hayo huku Marekani ikiendelea kutoa vitisho vya kuishambulia Venezuela na kulitaka jeshi la nchi hiyo lishirikiane na majeshi ya Marekani katika mapinduzi dhidi ya Rais Nicolas Maduro. 

Tarehe 19 Februari Rais Donald Trump wa Marekani alitoa vitisho dhidi ya wanajeshi wa Venezuela akisema kuwa, iwapo wataendelea kuwa watiifu kwa Maduro hawatakuwa na makimbilio ya amani wala njia ya kujiokoa. Matamshi hayo ya Trump yalikabiliwa na jibu kali la Waziri wa Ulinzi wa Venezuela. Vladimir Padrino López alisema: "Jeshi na makamanda wa vikosi vya Jenezuela hawapokee amri kutoka nchi za nje, na wapinzani wanapaswa kutambuka maiti za wanajeshi wa Venezuela kabla kuweze kumuondoa madarakani Rais Nicolas Maduro na kulazimisha serikali mpya."

Vladimir Padrino López

Kuendelea kwa mgogoro wa kisiasa wa Venezuela na kufeli kwa njama ya Marekani na waitifaki wake ya kutaka kufanya mapinduzi dhidi ya serikali halali ya nchi hiyo kumeifanya serikali ya Washington itoe vitisho vya kuishambulia nchi hiyo na kuwataka wanajeshi wajiunge la safu za wapinzani wa serikali. Mbinu hiyo ya Marekani inakusudia kuteteresha imani ya wanajeshi wa Venezuela kwa ajili ya kutaka kutimiza malengo ya Washington ya kusimika serikali kibaraka huko Caracas. 

Katika mkondo huo huo siku chache zilizopita afisa mmoja wa ikulu ya Rais wa Marekani, White House, alifichua kwamba, serikali ya Washington imefanya jitihada kubwa za kujaribu kuwasiliana na maafisa wa jeshi la Venezuela na kuwahamasisha kujitenga lakini wanajeshi hao wamekataa kushirikiana na Marekani. Hivyo maafisa wa serikali ya Washington wamekhitari kutumia mbinu ya vitisho dhidi ya jeshi la Venezuela.

Donald Trump

Sambamba na njama hizo, kiongozi wa upinzani aliyejitangaza kuwa rais wa Venezuela, Juan Guaido ambaye anasaidiwa na kuungwa mkono na Marekani na waitifaki wake, amelitaka jeshi la nchi hiyo kubadili misimamo yake na kumuunga mkono. Hata hivyo makamanda wa jeshi la Venezuela wamesisitiza kuwa, wataendelea kuheshimu katiba ya nchi na kumtii Rais halali wa Venezuela, Nicolas Maduro.

Msimamo huo imara wa jeshi la Venezuela umekwamisha njama zote za Marekani dhidi ya kiongozi halali wa Venezuela. Kwa kadiri kwamba, hata shehena ya mizigo iliyodaiwa ni misaada ya kibinadamu ya Marekani na washirika wake kwa wananchi wa Venezuela imelazimika kubakia katika mpaka wa Venezuela na Colombia baada ya Caracas kutuma jeshi maeneo ya mpakani. Suala hilo limewakasirisha sana wapinzani wa Maduro.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela, Jorge Arreaza pia amesema kuwa: Tunataka kuzuia vita vya ndani nchini kwetu na hatutaki mapinduzi yatakayosababisha vita na mapigano, jambo ambalo ndilo takwa la Marekani. Hatutairuhusu Marekani kufanya operesheni ya aina yoyote ya kijeshi nchini Venezuela. Jeshi na wananchi wa Venezuela watashirikiana kulinda nchi yao.

Jorge Arreaza

Trump na timu yake ndani ya White House wanaendelea kuwa matarajio ya kuliona jeshi la Venezuela likitimiza ndoto yao ya kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Nicolas Maduro. Hata hivyo inaonekana kuwa, ndoto hiyo haitatimia na jeshi na wananchi wa Venezuela wanaendelea kusimama ngangari kulinda katiba na nchi yao.                

Tags