Nchi za Ulaya zalikataa ombi la Marekani la kuzitaka zibakie Syria
Nchi za Ulaya zimelikataa ombi la Rais Donald Trump wa Marekani la kuzitaka zipeleke vikosi vya majeshi yao nchini Syria na kujaza nafasi itakayoachwa wazi na vikosi vya jeshi la Marekani.
Toleo la jana Alkhamisi la gazeti la Washington Post limezinukuu duru za kuaminika na kuandika kuwa, nchi za Ulaya zimetamka kwa kauli moja kuiambia Marekani kwamba 'kama nyinyi mtaondoka Syria, sisi hatutabakia.'
Nchi za Ulaya zimeshurutisha kuwepo kubaki kijeshi nchini Syria kwa kubaki angalau idadi fulani ya askari wa jeshi la Marekani nchini humo; na suala hilo limewafanya wabunge wa Kongresi ya Marekani, maafisa wa White House na wa Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo Pentagon wamtake Donald Trump atazame upya uamuzi wake kuhusiana na kuwaondoa askari wa nchi hiyo nchini Syria.
Kwa sasa, Uingereza na Ufaransa ndizo nchi pekee waitifaki wa Marekani zenye askari wao nchini Syria.
Mnamo mwezi Desemba 2018, na kwa maelezo kwamba kundi la DAESH limeshasambaratishwa nchini Syria, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa atawaondoa askari elfu mbili wa nchi hiyo katika ardhi ya Syria.
Katika kipindi cha miaka saba cha kuwepo kwake kijeshi kinyume cha sheria nchini Syria na kwa madhumuni ya kuwaunga magaidi, Marekani imeshindwa kulifikia lengo lake la kuiangusha serikali halali ya Damasacus na kuimarisha nafasi ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Mashariki ya Kati.
Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 kwa hujuma na mashambulio makali ya makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudi Arabia, Marekani na waitifaki kwa lengo la kubadilisha mlingano wa nguvu za kijeshi katika eneo kwa manufaa ya Israel, lakini njama hiyo imegonga ukuta kutokana na juhudi za jeshi na wananchi wa Syria.../