Trump adai hakuna ubaguzi wa rangi katika jamii za Magharibi
Katika hali ambayo hivi sasa dunia nzima inaomboleza mauaji ya kutisha yaliyotokea jana Ijumaa katika misikiti miwili nchini New Zealand kutokana na hisia kali za ubaguzi wa rangi na wa kizazi, rais wa Marekani, Donald Trump amejitokeza hadharani na kudai kuwa eti hakuna ubaguzi wa rangi katika jamii za Magharibi.
Gazeti la Washington Post limemnukuu Donald Trump akidai kuwa mashambulio ya jana Ijumaa dhidi misikiti miwili ya Linwood na Al-Noor katika mji wa Christchurch nchini New Zealand yaliyowalenga Waislamu waliokuwa wanasali Sala ya Ijumaa halikutokana na hisia za ubaguzi wa rangi. Katika jinai hiyo ya kinyama Waislamu 50 waliuawa na wengine 50 kujeruhiwa.
Trump alitumia fursa ya kikao cha kuupigia veto mpango wa kufuta hali ya hatari nchini Marekani kudai kuwa mashambulio ya mjini Christchurch huko New Zealand si ya ubaguzi wa rangi wala kizazi. Amma kuhusiana na matamshi ya mmoja wa magaidi waliofanya jinai hiyo huko New Zealand aliyesema kuwa ameathiriwa na misimamo ya Donald Trump, rais huyo wa Marekani amedai kuwa hana taarifa na jambo hilo.
Trump anaendelea kulaumiwa vikali kutokana na hatua yake ya kunyamazia kimya machafuko yaliyofanywa na magenge ya kibaguzi mwaka 2017 katika mji wa Charlottesville huko Virginia Marekani.
Vyombo vya habari vya Marekani vimefanananisha shambulio hilo la mwaka 2017 huko Virginia na shambulizi la jana la nchini New Zealand na kutahadharisha kuhusu kuongezeka chuki na mashambulizi dhidi ya Waislamu katika jamii za Magharibi.