Tishio la Marekani kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC)
https://parstoday.ir/sw/news/world-i52221-tishio_la_marekani_kwa_mahakama_ya_kimataifa_ya_jinai_(icc)
Tokea aanze kuitawala Mareakni, Rais Donald Trump amekuwa akikosoa vikali na kuonyesha dharau kubwa kwa taasisi za kimataifa. Trump ni mkosoaji na mpinzani mkubwa wa Umoja wa Mataifa na sera za umoja huo na amekuwa akitishia mara kwa mara kuwa Marekani itapunguza msaada wake wa kifedha kwa taasisi hiyo ya kimataifa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 17, 2019 04:22 UTC
  • Tishio la Marekani kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC)

Tokea aanze kuitawala Mareakni, Rais Donald Trump amekuwa akikosoa vikali na kuonyesha dharau kubwa kwa taasisi za kimataifa. Trump ni mkosoaji na mpinzani mkubwa wa Umoja wa Mataifa na sera za umoja huo na amekuwa akitishia mara kwa mara kuwa Marekani itapunguza msaada wake wa kifedha kwa taasisi hiyo ya kimataifa.

Kati ya hatua ambazo rais wa Marekani amechukua dhidi ya Umoja wa Mataifa ni kujiondoa katika taasisi muhimu za umoja huo kama vile UNESCO, Baraza la Haki za Binadamu na pia kukata misaada ya  Shirika la Umoja wa Mataifa la Kusaidia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA.

Katika hatua nyingine dhidi ya Umoja wa Mataifa, siku ya Ijumaa, Mike Pompeo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alisema kuwa, nchi hiyo itawawekea marufuku ya viza ya kuingia Marekani maafisa wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC watakAotaka kuwasaili na kuwachunguza wanajeshi wa nchi hiyo wanaotuhumiwa kufanya jinai za kivita.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema kuwa, nchi hiyo itawawekea marufuku ya viza ya kuingia Marekani maafisa wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai watakaotaka kuwasaili na kuwachunguza wanajeshi wa nchi hiyo wanaotuhumiwa kufanya jinai za kivita huko Afghanistan. Pompeo alibainisha zaidi kwa kusema: "Mimi leo ninatangaza kuwa, serikali ya Marekani itatekeleza sera ya kuweka vizuizi katika utoaji viza kwa watu ambao wanahusika moja kwa moja katika uchunguzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai dhidi ya wanajeshi wa Marekani."

Kwa utaratibu huo, Marekani inataka kuanza kuwaadhibu maafisa wa ICC ambao wanahusika kuchunguza jinai za kivita za askari wa Marekani huko Afghanistan na nchi zingine kwa kuwanyima visa ya kuingia Marekani.

ICC ni taasisi ya kisheria ambayo ina jukumu la kuchunguza faili za jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu. Mnamo Septemba 2018, Ikulu ya White House ilikosoa vikali ICC na kuwatisha majaji na waendesha mashtaka wa taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa kuwa endapo watawachunguza askari wa Marekani au Israel basi  watawekewa vikwazo. Pompeo hata hivyo hajatangaza ni maafisa wapi wa ICC watakaochukuliwa hatua.

Wanajeshi vamizi wa Marekani nchini Afghanistan

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda, mwanzoni mwa Novemba 2018 alitangaza kuwa ameomba idhini ya majaji wa mahakama hiyo ili aanzishe uchunguzi kuhusu uwezekano kuwa askari wa Marekani walitenda jinai za kivita nchini Afghanistan. Kufuatia ombi hilo la Bensouda, Marekani imekosoa vikali Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na imesisitiza kutoshirikiana na mahakama hiyo ya kimataifa.

John Bolton, mshauri wa usalama wa kitaifa wa Marekani alitoa tamko kufuatia uamuzi wa Mwendesha Mashtaka wa ICC kuhusu kuchunguzwa jinai za Marekani Afghanistan na kusema: "Hatutashirikiana na mahakama hii."

Hatua ya utawala wa Trump kupinga uchunguzi wa ICC kuhusu jinai za wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan ni ushahidi wa wazi kuwa Marekani inafahamu wanajeshi wake wamekuwa wakihusika na jinai nchini Afghanistan.

Marekani iliivamia na kuikalia kwa mabavu Afghanistan miaka 18 iliyopita kwa kisingizio cha kukabiliana na magaidi wa Al Qaeda na Taliban kufuatia mashambulio ya Septemba 11 mwaka 2001.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda

Pamoja na kuwa wanajeshi wa Marekani na waitifaki wake katika NATO wamekuwa Afghanistan kwa muda huo wote lakini nchi hiyo haijapata usalama wa maana. Kuwepo wanajeshi wa nchi za Magharibi huko Afghanistan hakujakuwa na matokeo yoyote ghairi ya kuuawa raia, kuharibiwa miundo msingi ya nchi hiyo, kuongezeka ugaidi na pia kuongezea ukulima wa mihadarati.

Ben Rhodes, aliyekuwa mshauri wa Barack Obama ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa: "Hatupaswi kuendelea na vita visivyokuwa na mwisho ambavyo malengo yake hayawezi kufikiwa."

Wanajeshi wa Marekani wametenda jinai chungu nzima katika muda wote ambao wamekuwa nchini Afghanistan na ni lazima waliohusika na jinai wafikishwe kizimbani na hatimaye waadhibiwe. 

Marekani inajihesabu kuwa yenye cheo maalumu duniani na inawatazama wanajeshi wake wanaotenda jinai kuwa walio na kinga ya kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa.