Waustria waandamana kupinga sera za kibaguzi dhidi ya Uislamu
Maelfu ya wakazi wa mji mkuu wa Austria, Vienna wamefanya maandamano wakipinga sera na siasa za mrengo wa kulia wenye misimamo ya kufurutu mipaka, za kibaguzi na dhidi ya Uislamu barani Ulaya.
Waandamanaji hao wanaokadiriwa kuwa elfu ishirini walikuwa na mabango yenye jumbe zinazosema: "Hatutaki sera za kinazi serikalini", "marufuku ya vazi la hijabu ni ya kibaguzi" na "ugaidi hauna dini".
Maandamano hayo yamefanyika baada ya mashambulizi ya kigaidi yaliyolenga misikiti ya Waislamu huko New Zealand na katika mji mkuu wa Uingereza, London.

Ijumaa iliyopita magaidi wenye chuki dhidi ya Uislamu walishambulia misikiti miwili ya Linwood na Al-Noor katika mji wa Christchurch nchini New Zealand na kuwamiminia risasi Waislamu waliokuwa wakiswali Swala ya Ijumaa. Katika hujuma hiyo ya kinyama Waislamu wasiopungua 49 waliuawa na wengine 50 kujeruhiwa. Nchi nyingi duniani na asasi za kimataifa hadi hivi sasa zinaendelea kulaani mashambulizi hayo.
Siku hiyo hiyo ya Ijumaa watu watatu wenye fikra za kuchupa mipaka walishambulia msikiti mmoja mjini London huko Uingereza na kutoa matusi na maneno machafu dhidi ya Uislamu.