Waingereza waandamana London kutaka kufanyika kura mpya ya maoni kuhusu Brexit
Mamia ya maelfu ya wananchi wa Uingereza wamefanya maandamano katika mji mkuu London, kushinikiza kufanyika kura mpya ya maoni kuhusu suala la kujitoa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya (Brexit).
Watu wa matabaka yote pasi na kujali mirengo yao ya kisiasa, walimiminika katika barabara za London jana Jumamosi kushiriki maandamano hayo.
Moja ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanaji hao lilikuwa na maandishi yanayosema "Samahani, unaweza kurudia tena swali?" Maandamano ya jana yaliitishwa na asasi ya kiraia inayojiita "Kura ya Wananchi".
Akitangaza uungaji mkono wa chama chake kuhusu suala la kufanyika kura mpya ya maoni kuhusu Brexit, Jeremy Corbyn, Mkuu wa Chama cha Labour amesema kuwa, chama hicho hakikubaliani na suala la Brexit bila ya kufikiwa mapatano kwa sababu jambo hilo litakuwa na maafa kwa Uingereza.
Siku chache zilizopita, mpango wa Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May wa kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya (EU) maarufu kama Brexit ulikataliwa kwa mara ya pili na bunge na kuitumbukiza nchi hiyo kwenye mtafaruku wa kisiasa huku zikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya tarehe rasmi ya utekelezaji wa mpango huo.
Wabunge wa Uingereza itawapasa wapige kura ya ama kujitoa katika Umoja wa Ulaya ifikapo Aprili 12 na wala sio Machi 29 kama ilivyokuwa imetangazwa hapo awali, au kuchelewesha mchakato huo.