Uchunguzi: Saudia ilidukua simu ya mmiliki wa Washington Post
https://parstoday.ir/sw/news/world-i52529-uchunguzi_saudia_ilidukua_simu_ya_mmiliki_wa_washington_post
Uchunguzi umefichua kuwa, Saudi Arabia ilidukua mawasiliano ya simu ya mmliki wa gazeti la Marekani la Washington Post, kutokana na gazeti hilo kuakisi kwa kina mauaji ya Jamal Khashoggi, aliyekuwa mwandishi wa habari na mkosoaji wa utawala wa Aal-Saud.
(last modified 2026-08-08T07:03:00+00:00 )
Mar 31, 2019 03:25 UTC
  • Uchunguzi: Saudia ilidukua simu ya mmiliki wa Washington Post

Uchunguzi umefichua kuwa, Saudi Arabia ilidukua mawasiliano ya simu ya mmliki wa gazeti la Marekani la Washington Post, kutokana na gazeti hilo kuakisi kwa kina mauaji ya Jamal Khashoggi, aliyekuwa mwandishi wa habari na mkosoaji wa utawala wa Aal-Saud.

Hayo yamefichuliwa na Gavin de Becker, mtaalamu wa usalama aliyepewa jukumu la kuendesha uchunguzi kuhusu uwezekano wa kudukuliwa mawasiliano ya simu ya mmliki wa  gazeti la Marekani la Washington Post ambaye pia ni Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya kiteknolojia ya Amazon ya Marekani, Jeff Bezos.

Mtaalamu huyo ameandika kwenye tovuti ya Daily Beast kuwa, "Utafiti wetu umebaini kuwa, kwa siri kubwa Saudia ilidukua mawasiliano ya simu ya Bezos na kupekua taarifa zake za siri kwa lengo la kumchafua."

Mmiliki wa gazeti hilo ambalo Khashoggi alikuwa akiliandikia makala mbali mbali amewahi kusema huko nyuma kuwa, 'Kitendo cha Washington Post kuakisi kwa mapana na marefu mauaji ya Khashoggi tena bila kuchoka, kiliwatia kiwewe watu fulani nchini', akikusudia wapambe na waitifaki wa Riyadh nchini Marekani.

Trump ameendelea kuukingia kifua utawala wa Riyadh licha ya jamii ya kimataifa kulaani mauaji ya kutisha ya Khashoggi

Khashoggi alitoweka katika mazingira ya kutatanisha baada ya kuingia katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki tarehe pili Oktoba mwaka jana. Hatimaye Saudia ililazimika kukiri tarehe 19 ya mwezi huo kwamba mwandishi huyo mkosoaji wa Riyadh aliuawa ndani ya ubalozi wake, kufuatia mashinikizo makali ya dunia, baada ya kuwa ilikadhibisha kwa mara kadhaa kuhusika kwa aina yoyote na jinai hiyo.

Jamal Khashoggi alikuwa katika orodha ya watu waliokuwa wanafuatiliwa na utawala wa Saudia kwa ajili ya kukamatwa.