Paris: Magaidi raia wa Ufaransa hawana ruhusa ya kurejea nchini
https://parstoday.ir/sw/news/world-i52550-paris_magaidi_raia_wa_ufaransa_hawana_ruhusa_ya_kurejea_nchini
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amesisitiza kuwa, hakuna gaidi yeyote raia wa Ufaransa atakayeruhusiwa kurejea nchini humo kutoka Syria na Iraq.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 01, 2019 02:29 UTC
  • Paris: Magaidi raia wa Ufaransa hawana ruhusa ya kurejea nchini

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amesisitiza kuwa, hakuna gaidi yeyote raia wa Ufaransa atakayeruhusiwa kurejea nchini humo kutoka Syria na Iraq.

Jean-Yves Le Drian amesema hayo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na gazeti la West-France la ufaransa na kuongeza kuwa, watu ambao ni Wafaransa lakini wamejiunga na magaidi wa Daesh (ISIS) kwa hakika wameipiga vita Ufaransa na ni maadui wa Ufaransa na hawana ruhusa ya kurejea nchini humo bali inabidi hukumu zao zitolewe na kutekelezwa huko huko Syria na Iraq.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa ameongeza kwamba, ijapokuwa magaidi wa Daesh wamepoteza ngome zao zote huko Iraq na Syria lakini bado ni tihsio kwa usalama wa dunia kwani magaidi hao bado wanaendesha operesheni zao chini kwa chini katika kona tofauti duniani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian

 

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ufaransa ameikosoa vikali pia Marekani kwa kutoheshimu maamuzi wa Umoja wa Mataifa akisema kuwa, Marekani inajifikiria peke yake na inaamini kuwa kutumia mabavu ndio njia ya kuwa na uhusiano na mataifa mengine duniani wakati ni makosa.

Vile vile amekosoa mtazamo wa Russia na China kwa Umoja wa Mataifa na kudai kuwa, nchi hizo zenye haki za veto katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hazisiti kutumia kura hiyo ya turufu katika kila jambo lisipowapendeza wao binafsi.

Ikumbukwe kuwa Jumanne iliyopita Ufaransa ilichukuwa uenyekiti wa mzunguko wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.