Yukiya Amano: Saudia ituwekee dhamana kuhusiana na miradi yake ya nyuklia
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) Yukiya Amano ameitaka Saudi Arabia kuweka dhamana za kiusalama kuhusiana na kinu chake cha kwanza cha nyuklia.
Amano ameyasema hayo Jumamosi ya jana na kusisitiza kwamba wakala huo unaitaka Riyadh kuweka dhamana hiyo kuhusiana na mada za nyuklia zilizoandaliwa kwa ajili ya kinu chake cha kwanza ambacho kunatazamiwa kufunguliwa mwishoni mwa mwaka huu. Ameongeza kwamba Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) unataka kuiona Saudia ikitoa dhamana jumla ya kimaandishi kuhusiana na kujiepusha kwake na uundaji wa silaha kwa kutokana na mada za nyuklia. Hayo yanajiri katika hali ambayo, gazeti la Raialyoum limeonyesha mchoro wa picha iliyochukuliwa na satalaiti ambayo kwa mujibu wake inaakisi mpango wa utekelezwaji wa miradi ya nyuklia katika viunga vya mji mkuu wa nchi hiyo 'Riyadh.'
Aidha tarehe 28 Machi Waziri wa Nishati wa Marekani, Rick Perry alitangaza habari ya kutolewa vibali sita kwa ajili ya kuiuzia Saudia teknolojia ya nyuklia na kushirikiana na nchi hiyo katika uwanja huo. Wakati huo huo, wawakilishi wa bunge la Marekani wameonyesha wasiwasi wao juu ya uwezekano wa nchi hiyo ya Kiarabu kumiliki silaha za nyuklia ambapo wameitaka serikali ya Rais Donald Trump ijiepushe na hatua ya kuipatia Saudia teknolojia ya nyuklia. Aidha tarehe Mosi mwezi Machi mwaka huu wawakilishi hao wa bunge la Marekani waliwasilisha muswada ambao kwa mujibu wake ushirikiano wowote kati ya Washington na Saudia unatakiwa ufanyike kwa kuzingatia kukubaliwa na bunge hilo. Marekani inaipatia Saudia teknolojia ya nyuklia katika hali ambayo kwa miaka kadhaa sasa, Washington na washirika wake wamekuwa wakipiga ngoma ya kutaka kuizuia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kustafidi ya miradi ya nyuklia ambayo inatumiwa hapa nchini kwa malengo ya amani kabisa.