Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani ajiuzulu
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani, Kirstjen Nielsen ambaye amekuwa akikosolewa vikali kwa kuongoza utekelezaji wa sera ya kikatili ya kuwatenganisha watoto wadogo na wazazi wao wahajiri katika mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Mexico amejiuzulu.
Rais Donald Trump wa Marekani amemteua Kevin McAleenan, Kamishna wa Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mpaka, kukaimu nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Kirstjen Nielsen.
Nielsen amejiuzulu siku mbili tu baada ya Trump kuutembelea mpaka wa pamoja wa Marekani na Mexico na kudai kuwa mgogoro wa wahajiri katika eneo hilo la kusini ni wa kutisha.
Asasi mbalimbali za kutetea haki za binadamu ikiwemo Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa zimekuwa zikiitaka serikali ya Marekani ikomeshe sera yake hiyo ya kikatili ya kuwatenganisha watoto wadogo na wazazi wao wahajiri katika mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Mexico.
Serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump kuanzia katikati ya mwezi Aprili mwaka jana hadi sasa imewatenganisha maelfu ya watoto na wazazi wao ambao wametiwa nguvuni kwa tuhuma za kuingia katika ardhi ya Marekani kinyume na sheria.
Trump amekuwa akishinikiza kutengewa dola bilioni tano na milioni 700 zinazohitajika kwa ajili ya ujenzi wa ukuta katika mpaka wa Mexico.