Trump avunja rekodi za makidhabu na wasema uongo duniani
Uchunguzi uliofanywa na mtandao mmoja wa kuchunguza ukweli umesema kuwa, rais wa Marekani, Donald Trump amevunja rekodi za wasema uongo kwa kusema uongo mara 23 kila masaa 24 katika kipindi cha miezi saba iliyopita.
Katika ripoti yake ya karibuni kabisa, gazeti la Washington Post limesema kuhusu tathimini iliyofanywa na mtandao mmoja wa kuchunguza ukweli juu ya matamshi ya Donald Trump kwamba, rais huyo wa Marekani hadi hivi sasa ameshatoa madai ya uongo elfu kumi na mia moja na kumi na moja (10,111) katika hotuba, ujumbe na matamshi yake tangu alipoingia madarakani huko Marekani.
Gazeti hilo la nchini Marekani limeandika kuwa, katika kipindi cha siku 601 za mwanzoni mwa urais wake, Trump alitoa zaidi ya madai elfu tano ya uongo na kwa wastani alisema uongo mara nane katika kila masaa 24.
Hata hivyo ilipofika tarehe 26 mwezi huu wa Aprili, yaani siku 226 tu tangu ilipotolewa ripoti kwamba alishasema uongo mara 5,000, rais huyo wa Marekani alivunja rekodi zote za kusema uongo. Mtandao wa Fact Checker wa gazeti la Washington Post unaonesha kuwa Trump amepindukia matamshi 10,000 ya uongo, yaani wastani wa madai 23 ya uongo kila siku katika kipindi cha miezi saba iliiyopita.
Itakumbukwa kuwa, gazeti la Washington Post lilifungua ukurasa maalumu wa kuchunguza ukweli unaoitwa Fact Checker, tangu Donald Trump alipoingia katika Ikulu ya White House na kazi ya mtandao huo ni kuchunguza madai ya mara kwa mara ya uongo yanayotolewa kiholela na rais huyo wa Marekani.
Mtandao huo umeongeza kuwa, katika kipindi cha siku 100 za Ikulu, Trump alikuwa ametoa matamshi yasiyofika hata matano ya uongo na kama angeliendelea hivyo angelikuwa na wastani wa madai 7,000 ya uongo katika kipindi chote cha miaka minne ya uongozi wake. Hata hivyo baada ya siku hizo mia moja, tsunami ya madai ya uongo yanayotolewa na Trump ilianza na kila siku zinavyopita ndivyo tsunami hiyo inavyozidi kuwa kubwa.