Aug 06, 2019 03:00 UTC
  • Tahadhari ya kuenea ugaidi wa ndani nchini Marekani

Hata kama kufuatia mashambulio ya Septemba 11, 2001 Marekani ilijitangaza kuwa mbeba bendera wa mapambano dhidi ya ugaidi ulimwenguni na kufanya uvamizi wa kijeshi katika nchi kadhaa kwa kisingizio hicho, lakini kuongezeka kwa kesi za mashambulio ya silaha nchini humo na hasa katika siku chache zilizopita, kumepelekea kutolewa tahadhari kali juu ya kuongezeka ugaidi wa ndani katika nchi hiyo ya Magharibi.

Katika tukio la kwanza siku ya Jumamosi lililotekelezwa kwa kisingizio cha kupambana na wahajiri haramu wanaotoka katika nchi za Amerika ya Latini, kijana mmoja mwenye umri wa miaka 21 alifyatua risasi kiholela na kuwaua watu 20 katika mji wa El Paso ulioko katika jimbo la Texas linalopakana na Mexico. Kabla ya kutekeleza jinai hiyo, kijana huyo mkazi wa Dallas alisambaza katika moja ya mitandao ya kijamii ujumbe uliojaa chuki na mitazamo ya kibaguzi dhidi ya wageni na watu wasiokuwa weupe. Katika tukio la pili siku hiyo hiyo, kijana mwingine mwenye umri wa miaka 24 alifyatua risasi na kuwaua watu 10 wasio na hatia katika mji wa Dayton katika jimbo la Ohio. Matukio hayo ya jinai ambayo yameorodheshwa na Polisi ya Federali ya Marekani kuwa ya kigaidi, yamepelekea kuongezaka tahadhari za kuenea ugaidi wa ndani nchini Marekani.

Katika uwanja huo, wakurugenzi sita wa zamani wa ngazi za juu katika Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani wametoa taarifa wakiyataja matukio ya hivi karibuni ya mauaji nchini humo kuwa ya kigaidi na kutaka hatua za dharura zichukuliwe na serikali kwa ajili ya kupambana na tatizo hilo.

Mauji ya karibumi huko El Paso Texas

Joshua Glitzer mmoja wa wakurugenzi hao wa zamani wa ngazi za juu aliyehudumu katika baraza hilo tokea mwaka 2015 hadi 2017 ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twiter kwamba: Yapata mwaka mmoja uliopita, ambapo serikali ya Trump alisambaza stratejia ya kwanza ya kitaifa ya kupambana na ugaidi, sote tulifurahia jambo hilo kutokana na kutambua kwake udharura wa kuongezwa juhudi za kupambana na kile kilichotajwa na wengi kuwa ugaidi wa ndani, ambao ulikuwa na maana ya ugaidi unaotekelezwa katika ardhi ya Marekani bila ya kuwa na uhusiano wowote na makundi ya kimataifa ya kigaidi kama vile Daesh na al-Qaida.

Anakiri kwamba matukio ya hivi karibuni yanathibitisha kuwa juhudi za ziada zinapasa kufanywa kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya mabavu vinavyotokana na mitazamo ya kupindukia mipaka ukiwemo ugaidi wa ndani. Wakurugenzi hao wa zamani wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani wanasema kwamba mapambano dhidi ya ugaidi wa ndani yanapaswa kupewa uzito kama ule unaotelewa kwa mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa, kama ilivyoainishwa katika stratejia ya taifa ya mapambano dhidi ya ugaidi, iliyotangazwa mwaka uliopita na serikali ya Rais Donald Trump.

Mizizi ya ugaidi wa ndani nchini Marekani inarudi nyuma makumi ya miaka ambapo kuna makundi na watu waliotekeleza mashambulizi makubwa ya kigaidi nchini humo.  Moja ya matukio hayo ni mlipuko mkubwa wa kigaidi uliotokea katika Jengo la Federali la Alfred Murrah tarehe 19 Aprili 1995 ambao ulitekelezwa na makundi ya wanamgambo wa ndani waliokuwa wanalalamikia siasa za serikali kuu ya Marekani.

Mtenda jinai aliyehusika na mauaji ya Dayton, Ohio

Hivyo mizizi ya ugaidi wa ndani nchini Marekani inapaswa kutafutwa miongoni mwa makundi ya wanamgambo wa nchi hiyo, ambayo mengi yana misimamo ya mirengo ya kulia. Wanamgambo hao ni pamoja na wale wanaopigania serikali za majimbo kupewa madaraka makubwa zaidi ya kujitawala, wapinzani  wa siasa za serikali kuu, makundi ya wabaguzi wa rangi na dini na wale walio na mitazamo ya mirengo ya kulia wanaopinga uhamiaji wa wageni na kutaka jamii ya watu weupe ipewe fursa na upendeleo maalumu juu ya jamii nyinginezo za Marekani. Kama tunavyoona, Patrick Crusius, muhusika wa mauaji ya hivi karibuni huko El Paso alikuwa na mitazamo inayopinga wazi wahajiri na kuunga mkono moja kwa moja siasa zilizo dhidi ya wahajiri za Rais Trump wa nchi hiyo. Kuhusiana na suala hilo, Pete Buttigieg na Beto O'Rourke wagombea wawili wa kiti cha rais wa Marekani katika uchaguzi ujao wa mwaka 2020 kwa tiketi ya chama cha Democrat, wamesema wazi wazi kwamba misimamo ya ubaguzi wa rangi ya Trump ndiyo imechochea vitendo hivyo vya ubaguzi. Pete Buttigieg anasema: Marekani inashambuliwa kigaidi na watu weupe walio na mitazamo ya ubaguzi wa rangi na utaifa ambao wanachochewa na Rais Donald Trump. Naye Beto O'Rourke anasema: Katika kipindi chote cha miaka mitatu ya urais wa Trump tumekuwa tukishuhudia kuongezeka jinai zinazotokana na chuki za kijamii. Kipindi ambacho rais wa nchi amekuwa akiwatukana Wamexico kuwa ni wabakaji na wahalifu.

Onyo na tahadhari ya wakurugenzi wa zamani wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani imetolewa kwa kutilia maanani kuongezeka nchini humo vitendo vya jinai, ambao ni ugaidi moja kwa moja.

Tags