Hasira zapanda Uingereza baada ya waziri mkuu kusitisha vikao vya bunge
https://parstoday.ir/sw/news/world-i55688-hasira_zapanda_uingereza_baada_ya_waziri_mkuu_kusitisha_vikao_vya_bunge
Hasira zinaendelea kupanda miongoni mwa wananchi na wanasiasa nchini Uingereza baada ya waziri mkuu wa nchi hiyo kuchukua uamuzi wa kidikteta wa kusitisha vikao vya bunge.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Aug 30, 2019 03:31 UTC
  • Hasira zapanda Uingereza baada ya waziri mkuu kusitisha vikao vya bunge

Hasira zinaendelea kupanda miongoni mwa wananchi na wanasiasa nchini Uingereza baada ya waziri mkuu wa nchi hiyo kuchukua uamuzi wa kidikteta wa kusitisha vikao vya bunge.

Siku ya Jumatano, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson alitangaza kuwa Bunge la Uingereza litasitisha vikao vyake hadi Oktoba 14. Sawa na siku kumi na tano kabla ya tarehe iliyopangwa ya Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya (Brexit). Hatua hiyo inalenga kulizuia bunge kujadili maudhui hiyo ya Brexit. Upinzani umelaani hatua hiyo na kuitaja kuwa ni ya kidikteta, huku ukimshtumu Boris Johnson kwamba lengo lake ni kuwanyamazisha wabunge ili afikie ndoto yake ya kutaka Uingereza ijitoe katika Umoja wa Ulaya bila mkataba.

Mbunge Bi. Nicola Sturgeon mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Skotland amesema uamuzi huo wa Johnson utakumbukwa katika historia ya Uingereza kama siku ambayo demokrasia ya Uingereza iliangamia. Naye kiongozi wa chama cha upinzani cha Leba Jeremy Corbyn amesema uamuzi huo ni tishio kwa demokrasia na amemuandikia barua Malikia Elizabeth akitaka mkutano wa dharura. Bunge la Uingereza linafungwa kwa muda baada ya Malikia Elizabeth kuafikiana kuhusu uamuzi huo wa Johnson.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson na Malikia Elizabeth ambao hawajapigiwa kura na wananchi wameamua kusitisha vikao vya bunge

Raia milioni moja na nusu wa Uingereza tayari wameshatia saini waraka wa kutaka vikao vya bunge viendelee kama kawaida.

Wakosoaji wanasema Waziri Mkuu  Boris Johnson na Malikia Elizabeth, ambao hawajachaguliwa kwa kura za wananchi,  wamechukua uamuzi wa kusitisha vikao vya wabunge waliochaguliwa moja kwa moja na wananchi, ili kukandamiza mijadala kuhusu Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya.