India yawazuia Waislamu wa Kashmir kumuomboleza Imam Hussein AS
India imetangaza sheria ya kutotoka nje katika baadhi ya maeneo ya Kashmir, sambamba na kuwapiga marufuku Waislamu wa madhehebu ya Shia katika eneo hilo inalolidhibiti kushiriki katika marasimu yoyote ya kidini.
Duru za habari zinaarifu kuwa, New Delhi imechukua hatua hiyo kwa lengo la kuwazuia Waislamu wa madhehebu ya Shia kushiriki hafla za maombolezo ya Imam Hussein AS ambazo kilele chake ni katika siku za Tasu'a (leo Jumatatu) na Ashura kesho Jumanne.
Jana Jumapili, magari ya polisi huku yakitumia vipaza sauti yalizunguka mitaani yakitangaza marufuku hiyo katika maeneo ya Lal Chowk mjini Srinagar.
Tangu Jumamosi, maafisa wa polisi ya India wamekuwa wakiwashambulia wakazi wa maeneo ya Rainawari na Badgam katika mji huo wa Srinagar kwa tuhuma za kukiuka marufuku hiyo, maeneo ambayo aghalabu ya wakazi wake ni Waislamu wa Shia.
Ifahamike kuwa, sehemu moja ya Kashmir iko chini ya udhibiti wa India na nyingine iko Pakistan. Nchi zote mbili zinadai kuwa wamiliki wa Kashmir yote.
Wakaazi wa eneo la Kashmir linalotawaliwa na India wanataka kura ya maoni iainishe hatima yao ya ima kubakia India, kupata uhuru kamili au kujiunga na Pakistan, pendekezo linalopingwa vikali na India.