Uingereza yakiuka marufuku ya kuiuzia silaha Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i56073-uingereza_yakiuka_marufuku_ya_kuiuzia_silaha_saudia
Serikali ya Uingereza imekiri kuwa ilikiuka marufuku ya kuuzia silaha utawala wa Aal-Saud wa Saudi Arabia unaoua raia wasio na hatia huko Yemen.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 18, 2019 02:39 UTC
  • Uingereza yakiuka marufuku ya kuiuzia silaha Saudia

Serikali ya Uingereza imekiri kuwa ilikiuka marufuku ya kuuzia silaha utawala wa Aal-Saud wa Saudi Arabia unaoua raia wasio na hatia huko Yemen.

Waziri wa Biashara ya Kimataifa wa Uingereza, Liz Truss, amelazimika kuiomba radhi mahakama, kutokana na hatua ya serikali ya London ya kukiuka agizo la chombo hicho cha sheria la kutaka kusitishwa mauzo hayo. 

Amekiri kuwa, hatua ya hivi karibuni ya serikali ya Uingereza ya kuidhinisha mauzo ya zana za kijeshi zenye thamani ya Pauni 435,200 kwa Saudia ilikiuka wazi wazi agizo hilo la mahakama.

Serikali ya Kihafidhina nchini Uingereza licha ya uamuzi wa mwezi Juni mwaka huu wa Mahkama ya Rufaa wa kupinga mauzo hayo, lakini bado serikali hiyo inaendelea kuiuzia Saudia silaha.

Marekani na Uingereza zinaongoza katika orodha ya kurundika silaha Saudia

Mapema mwezi huu, uchunguzi mpya uliofanywa na timu ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa ulieleza kuwa, kutokana na kuusaidia muungano wa Saudia kwa taarifa za kiintelijensia na kilojistiki mbali na silaha, Marekani, Ufaransa na Uingereza ni washirika wa jinai za kivita dhidi ya wananchi wasio na hatia wa Yemen.

Tangu vilipoanza vita vya Yemen mwezi Machi 2015, serikali ya Uingereza ilitoa kibali cha mauzo ya silaha zinazokaribia Pauni bilioni tano kwa Saudia, kama ambavyo pia imekuwa na nafasi chanya katika kutoa mafunzo kwa askari wa utawala huo wa kifalme.