Safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran mjini London
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif leo yuko mjini London, kufuatia mwaliko rasmi wa mwenzake wa Uingereza Phillip Hammond, kushiriki katika kikao cha kimataifa cha kuisaidia Syria na Mashariki ya Kati.
Kikao hicho cha leo Alhamisi kimeandaliwa kwa pamoja na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron. Kikao hicho kinatarajia kukusanya misaada ya kuwasaidia kifedha watu wa Syria na wakimbizi wa ndani na nje ya nchi hiyo. Hali kadhalika mkutano huo unajadili njia za kuwapa ajira wakimbizi na kuwaelimisha takribani watoto laki saba wa Syria ambao ni wakimbizi. Umoja wa Mataifa umesema unahitaji takribani dola bilioni 7,730 kuwasaidia watu wa Syria mwaka huu.
Mwaka uliopita watu wa Syria walihitaji msaada wa takribani dola bilioni saba lakini ni nusu tu ya misaada hiyo ndiyo iliyoweza kupatikana.
Misaada ambayo inajadiliwa sasa ya kuwasaidia wakimbizi wa Syria ni ya muda mfupi tu. Hii ni katika hali ambayo utatuzi wa kadhia ya wakimbizi wa Syria ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kurejea nchini kwao ni kadhia ambayo itachukua miaka mingi. Kwa msingi huo, mpango wa kuwapa ajira na elimu wakimbizi Wasyria ni kati ya maudhui muhimu zaidi za kikao cha leo cha London.
Hatua kama hizi za kutoa misaada ya kifedha ni muhimu lakini muhimu zaidi ya hilo ni utatuzi wa mgogoro wa Syria na kusitisha wimbi la wakimbizi wa nchi hiyo na Iraq ambao wanatoroka nchi zao kutokana na ukatili wa makundi ya kigaidi.
Baadhi ya madola ya Kimagharibi na waungaji mkono wengine wa makundi ya kigaidi wanazidisha mashinikizo ya kisiasa na kijeshi kwa serikali ya Syria ili kuilazimu ikubali matakwa ya magaidi. Syria hivi sasa inakabikiwa na mashinikizo ya pande kadhaa. Mashinikizo hayo yalizidishwa wakati jeshi la nchi hiyo lilipoanza kupata mafanikio katika medani ya vita sambamba na kufanikiwa ndege za kivita za Russia kutoa pigo kubwa kwa magaidi wa Daesh au ISIS.
Ukweli ni kuwa, tatizo la wakimbizi ni zito sana na limezidi kuwa baya zaidi kutokana na sera za kuwabana wakimbizi katika nchi za Ulaya mwezi uliopita. Nchi za Ulaya zimeidhinisha kutoa misaada kwa wakimbizi walioko nchini Syria lakini hazijatekeleza kivitendo uamuzi huo. Aidha ikumbukwe kuwa Uturuki na Saudi Arabia ndio waungaji mkono wakuu wa makundi ya kigaidi kama vile Daesh au ISIS. Kwa hivyo kutowasaidia wakimbizi na kuendelea kuunga mkono magaidi ni mambo yanayopelekea kuwa mbaya zaidi mgogoro na matatizo ya Syria.
Katika upande mwingine, Saudi Arabia inahusika moja kwa moja katika kuibua mgogoro na kuvuruga jitihada za kieneo za kutatua matatizo ya Syria. Uturuki nayo pia inahusika katika kuchochea mgogoro na kudhoofisha jitihada za Syria za kukabiliana na kundi la kigaidi la ISIS kwa kutoa visingizio na madai yasiyo na msingi. Kwa maelezo hayo, tatizo la wakimbizi linapaswa kuangaziwa kwa mtazamo mpana. Hii ni kwa sababu hali waliyojipata ndani wakimbizi inatokana na sera za nchi ambazo zinalenga kuiangusha serikali ya Syria na kuligawa vipande vipande eneo la Mashariki ya Kati. Hakuna mkimbizi anayependa hali iliyomsibu ya kuacha kila kitu chake na kuikimbia nchi.
Kwa msingi huo kikao cha London kinapaswa kuzingatia jitihada za Umoja wa Mataifa katika kutatua mgogoro wa Syria. Kuna udharura wa kuchukuliwa maamuzi ya kutatua mgogoro wa Syria na fauka ya hayo kuwepo jitihada za haraka za kumaliza vita na kuangamiza ugaidi katika eneo.