Onyo la kamanda wa jeshi la India kwa Pakistan
Kamanda wa jeshi la India ameituhumu serikali ya Pakistan kuwa inaunga mkono ugaidi.
Bipin Rawat amesema kuwa, umefika wakati kwa serikali ya India kuzingatia zaidi eneo la Kashmir linalodhibitiwa na Pakistan na kwamba jeshi la India limejiandaa kulikomboa eneo hilo. Mwezi uliopita kamanda wa jeshi la India pia alitangaza kwamba jeshi la nchi hiyo linajiandaa kutekeleza amri ya serikali ya New Delhi kwa ajili ya kulikomboa eneo hilo la Kashmir. Kama hiyo haitoshi S Jaishankar, Waziri wa Mambo ya Nje wa India siku ya Jumanne akiwa katika kikao na waandishi wa habari alinukuliwa akisema kuwa, eneo la Kashmir linalodhibitiwa na Pakistan, ni sehemu ya ardhi ya India na kwamba, serikali ya New Delhi inatumai kuwa siku moja itaweza kutekeleza katiba ya nchi hiyo katika eneo hilo. Matamshi ya kamanda huyo wa jeshi la India yametolewa katika hali ambayo, kitendo cha serikali ya India cha kulifutia mamlaka yake eneo la Jammu na Kashmir, kimeibua hasira kali kwa serikali na raia wa Pakistan. Aidha matamshi ya Bipin Rawat kwamba jeshi la India limejiandaa kwa ajili ya kudhibiti eneo la Kashmir linalotawaliwa na Pakistan, na ambayo yametolewa baada ya serikali ya New Delhi kukabiliwa na mashinikizo na radimali kali kutoka kwa jamii ya kimataifa kufuatia hatua yake yenye utata ya kulifutia mamlaka eneo la Jammu na Kashmir, ni aina fulani ya njama za India zenye lengo la kupotosha haki za msingi za wakazi Waislamu wa eneo hilo.
Aidha wakati kiongozi wa juu wa kijeshi nchini India anadai kuwa jeshi la nchi hiyo limejiandaa kulikomboa eneo la Kashmir linalodhibitiwa na Pakistan, wakazi wa Kashmir iliyo chini ya udhibiti wa Pakistan, hawana nia yoyote ya kuondoka katika udhibiti wa serikali kuu ya Islamabad. Badala yake wakazi Waislamu wa Kashmir iliyo chini ya udhibiti wa India na kwa miongo kadhaa wamekuwa wakitaka kufanyike kura ya maoni katika eneo hilo ili wapate fursa ya kutumia haki yao ya msingi katika kuainisha mustakbali wao, jambo ambalo limekuwa likipingwa vikali na serikali tofauti za India. Matakwa ya Waislamu wanaodhulumiwa wa Kashmir iliyo chini ya India ya kufanyika kura ya maoni eneo hilo, yanaungwa mkono pia na jamii ya kimataifa. Hii ni kusema kuwa, kwa mujibu wa azimio la Umoja wa Mataifa, serikali ya India inatakiwa kuandaa mazingira yanayofaa kwa ajili ya kufanyika kura hiyo ndani ya eneo hilo. Katika mazingira hayo, matamshi ya kamanda wa jeshi la India juu ya utayarifu wa jeshi la nchi hiyo wa kudhibiti eneo la Kashmir linalodhibitiwa na Pakistan na kisha kutekeleza katika eneo hilo katiba ya India, ni kinyume kabisa na mikataba na sheria za kimataifa, kama ambavyo pia yanapingana na matakwa ya wakazi wenyewe wa Kashmir inayodhibitiwa na Pakistan.
Katika hali ambayo kamanda wa jeshi la India anadai kuwa jeshi la nchi yake limejiandaa kutumia nguvu kwa ajili ya kulidhibiti eneo la Kashmir linalodhibitiwa na Pakistan, serikali ya New Delhi inatakiwa kuheshimu mitazamo ya wananchi na kujiepusha kuwatwisha uongozi wasiouridhia wakazi wa eneo hilo. Kwa sasa serikali ya India inakabiliana na wimbi la malalamiko makubwa ya wakazi wa Jammu na Kashmir, hasa baada ya kutekeleza hatua ya kijeshi ya kulifutia eneo hilo mamlaka yake ya ndani, ambapo inadhani kwamba kwa kuwaweka wakazi wa Kashmir katika kifungo cha ndani, itawalazimisha kukubali mazingira mapya ya kisiasa, kiusalama, kiuchumi na kijamii, siasa ambazo hazina faida yoyote ghairi ya kushadidisha mapambano na chuki ya wakazi wa eneo hilo dhidi ya serikali ya New Delhi. Kufuatia matokeo hatari ya kuendelea utawala wa kijeshi katika eneo la Kashmir, mahkama kuu ya India hivi karibuni iliitaka serikali ya New Delhi ihitimishe utawala huo wa kijeshi na kurejesha hali ya kawaida katika eneo hilo.