Askari wa Bangladesh wambaka binti wa miaka 12 wa Rohingya
Jeshi la Bangladesh limesema kuwa linachunguza malalamiko ya familia moja ya Waislamu wa Rohingya inayoishi katika kambi ya wakimbizi nchini humo inayosema kuwa askari wa Bangladesh wamembaka binti yao wa miaka 12.
Mohammad Osman, kaka mkubwa wa kiume wa binti huyo anayedaiwa kunajisiwa ameliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya simu kuwa, "Wanajeshi watatu wa Bangladesh waliingia katika nyumba yetu ya mabanda Jumapili iliyopita katika kambi ya Nayapara na kumbaka dadangu wa miaka 12."
Amesema askari mmoja alimfumba mdomo binti huyo ili asiweze kupiga nduru wakati wakimfanyia uchafu huo.
Msemaji wa jeshi la Bangladesh, Luteni Kanali Abdullah ibn Zaid amesema wanachunguza madai hayo na kwamba iwapo itabainika kuwa ni kweli tukio hilo lilifanyika, wahusika watakabiliwa na mkono wa sheria.

Katika kikao cha 74 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika mjini New York hivi karibuni, serikali ya Bangladesh ilitoa wito kwa jamii ya kimataifa ichukue hatua za kivitendo kutatua mgogoro wa wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya ambao wamelazimika kutafuta hifadhi nchini humo kutokana na mauaji ya kimbari ambayo yamekuwa yakitekelezwa dhidi yao huko Myanmar.
Kuanzia Agosti 25 mwaka 2017, Waislamu wapatao 740,000 wa jamii ya Rohingya walilazimika kuyahama makazi yao kwa umati katika jimbo lao la Rakhine nchini Myanmar na kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh walikojiunga na wenzao wengine laki mbili waliokuweko nchini humo, baada ya Mabuddha wenye misimamo mikali na vikosi vya jeshi la Myanmar kuanzisha wimbi kubwa la hujuma, ukandamizaji na mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu hao.