Oct 23, 2019 13:14 UTC
  • Takwimu: Watu wanaojiua wazidi kuongezeka nchini Marekani

Vyombo vya habari nchini Marekani vinaripoti kuwa, vitendo vya kujiua vimeongezeka mno nchini humo hususan baina ya vijana.

Mtandao wa habari wa National Interest umeandika kuwa, kwa mujibu wa takwimu za kituo cha kudhibiti na kukabiliana na maradhi mbalimbali kiwango cha kujiua miongoni mwa vijana nchini Marekani kimeongezeka kwa asilimia 56 katika kipindi cha miaka kumi ya hivi karibuni.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, kiwango cha kujiua baina ya watu wenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 24 kilifikia asilimia 6 hadi 10 katika kila watu laki moja mwaka 2017 kutoka asilimia 6 hadi 8 kati ya watu laki moja mwaka 2007.

Watu mashuhuri waliojiua  nchini Marekani hivi karibuni. Ingawa nyuso zao zina bashasha lakini inaonekana majonzi na kukata tamaa kuligubika nyoyo zao

Aidha ripoti hiyo inabainisha kuwa, katika kipindi hiki cha miaka kumi kiwango cha kujiua miongoni mwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 10 hadi 14 kiliongezeka mara tatu.

Wakati huo huo, kujiua ilitajwa kuwa sababu ya pili kuu ya vifo nchini Marekani katika mwaka 2017.

Aidha katika miaka kadhaa ya hivi karibuni watu wengi maarufu wamejiua nchini Marekani akiwemo Scott Stearney, kamanda wa wanajeshi wa Marekani walioko Bahrain, Robin Williams, mcheza filamu maarufu wa Hollywood, Anthony Bourdain, mmoja wa watangazaji maarufu wa televisheni ya CNN na Kate Spade mmoja wa wanamitindo wakubwa nchini Marekani.

Tags