Rais wa Ufaransa atuhumiwa kueneza chuki dhidi ya Waislamu
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametuhumiwa kuhusika na kueneza chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu katika nchi hiyo ya Ulaya.
Gazeti la Kifaransa la Le Figaro limeandika kuwa, Jean-Luc Antoine Pierre Mélenchon, mwenyekiti wa chama cha La France Insoumise (Ufaransa Haisalimu Amri) amesema Macron anachochea chuki dhidi ya Waislamu Ufaransa. Aidha amesema rais huyo wa Ufaransa anaibua utata kuhusu vazi la staha la Hijabu ambalo huvaliwa na wanawake Waislamu.
Baada ya mbunge mmoja wa Ufaransa kumvunjia heshima mwanamke Mwislamu ambaye alikuwa amevaa Hijabu, Macron alimuunga mkono mbunge huyo mwenye chuki dhidi ya Uislamu na kusema suala la Hijabu haliihusu serikali yake.

Katika upande mwingine, Bunge la Kitaifa la Ufaransa siku kadhaa zilizopita lilipasisha muswada dhidi ya Hijabu ambao umependekezwa na chama chenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia, Parti républicain.