Rais wa Ujerumani akosoa sera za kijuba za Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57189-rais_wa_ujerumani_akosoa_sera_za_kijuba_za_marekani
Siasa za kijuba na misimamo inayokiuka sheria za kimataifa ya Marekani imekuwa ikipingwa na kukosolewa na nchi nyingi duniani na hata washirika wa nchi hiyo barani Ulaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 11, 2019 03:35 UTC
  • Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier
    Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier

Siasa za kijuba na misimamo inayokiuka sheria za kimataifa ya Marekani imekuwa ikipingwa na kukosolewa na nchi nyingi duniani na hata washirika wa nchi hiyo barani Ulaya.

Kushika madaraka Donald Trump kama rais wa Marekani tarehe 20 Januari mwaka 2017 kulihuisha tena sera za kujichukulia siasa za upande mmoja za Marekani. Akitumia kaulimbiu ya "Marekani Kwanza", Donald Trump amekuwa akiweka mbele maslahi na malengo ya nchi hiyo na kupuuza kabisa maslahi ya nchi nyingine akiamini kwamba, siasa hizo za kijuba zitazidisha uwezo na nguvu ya Washington dhidi ya wapinzani wake. Siasa na sera hizi zimekabiliwa na upinzani mkali katika uga wa kimataifa. Katika mkondo huo Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier amekosoa siasa hizo za Marekani katika hotuba yake iliyotolewa kwa mnasaba wa kutimia miaka 30 baada ya kuvunjwa ukuta wa Berlin. Ameashiria siasa za Donald Trump za kupuuza maslahi ya nchi nyingine na msimamo wake wa kujenga ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico na kusema: Ujerumani ina hamu kubwa ya kuona uhusiano wa pande mbili za bahari ya Antlantic ukirejea katika hali yake ya awali. Ujerumani pia imeeleza masikitiko yake kutokana na uamuzi wa Marekani wa kujiondoa katika mkataba wa hali ya hewa wa Paris. Waziri wa Mazingira wa Ujerumani, Svenja Schulze amesema: Miaka miwili iliyopita Marekani ilijiondoa katika mkataba wa kimataifa wa hali ya hewa uliopasishwa na nchi zote duniani lakini kwa bahati nzuri imebakia peke yake katika suala hilo. 

Svenja Schulze 

Donald Trump amekuwa akitekeleza sera ya makusudi ya kuharibu taasisi zote za sera ya kuwepo mfumo wa kambi kadhaa duniani. Kiongozi huyo ambaye misimamo yake imekuwa ikizusha mijadala mingi katika uga wa kimataifa, anafanya mikakati ya kuimarisha mfumo wa kambi moja kwa kuiondoa nchi hiyo katika mikataba na makubaliano ya kimataifa. Awali aliiondoa Marekani katika mkataba wa kimataifa wa hali ya hewa wa Paris kisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yaliyopasisha na Umoja wa Mataifa. Trump pia ameanzisha jitihada za kuiondoa nchi hiyo katika makubaliano yote ya kudhibiti silaha na tayari ameiondoa Marekani katika Mkataba wa Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati (ANF). 

Trump pia ameiondoa Marekani katika Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) na katika Baraza la Haki za Binadamu la umoja wa huo. Trump hakutosheka na hayo na sasa ameanzisha vita vya kibiashara na nchi kadhaa hususan China na kuzua maswali mengi juu ya uhusiano wa Washington na shirika la kijeshi la nchi za Magharibi, NATO.

Kuhusiana na sera hizi za Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian anasema: Trump aliingia White House kwa kaulimbiu ya "Marekani Kwanza" lakini sasa amekwenda mbali zaidi na anaweka mbele kaulimbiu ya "Marekani Pekee". Paris inaamini kuwa, Ulaya inapaswa kubadili sheria zake kwa ajili ya kuanzisha sera mpya ya kambi kadhaa katika mahusiano yake na Marekani.

Jean-Yves Le Drian

Upinzani dhidi ya sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani hauishii katika nchi za Ulaya. Wapinzani wawili wakubwa wa Washington katika masuala ya kisiasa, kijeshi na kiuchumi duniani yaani Russia na China pia wamepaza sauti wakipinga vikali sera hizo za Donald Trump hususan katika masuala ya kimataifa.

Kwa sasa kumejitokeza kambi kubwa duniani inayopinga vikali sera na siasa hizo za kijuba za serikali ya Marekani na ukweli huo unaonekana katika msimamo wa jamii ya kimataifa dhidi ya hatua ya Donald Trump kuhusu ushuru wa forodha, vita vya kibiashara dhidi ya nchi nyingine, kujiondoa kwa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na mapatano ya hali ya hewa ya Paris na vilevile misimamo ya Trump kuhusiana na Quds (Jerusalem) na uhasama wake dhidi ya taifa la Palestina.