CIA: Akiba ya fedha za kigeni ya Saudia imekaribia kumalizika
Mkuu wa zamani wa Shirika la Kijasusi la Marekani, CIA amesema kuwa, akiba ya fedha za kigeni ya Saudi Arabia inaelekea kumalizika.
David Petraeus alisema hayo jana kwenye mahojiano na televisheni ya CNBC ya Marekani kuhusiana na malengo ya mwaka 2030 ya Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia na kusema kuwa, nakisi ya bajeti serikalini pamoja na Saudia kujiingiza kwenye vita hivi na vile katika eneo la Asia Magharibi ni miongoni mwa mambo yaliyopelekea kukaribia kumalizika utajiri wa nchi hiyo na kuangamia pole pole.
Ameongeza kuwa, nakisi ya bajeti ya Saudi Arabia hivi sasa kwa kuzingatia bei ya mafuta ni baina ya dola bilioni 40 hadi 60 kila mwaka huku nchi hiyo ikiwa inatumia fedha nyingi sana katika masuala ya ndani ya nchi za eneo hilo.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa zamani wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA, Wasaudia wanahitajia fedha na uwekezaji wa kigeni kuweza kufikia malengo yao ya mwaka 2030.
Matatizo ya kiuchumi ya Saudi Arabia yameongezeka katika miaka ya hivi karibuni huku wakuu wa nchi hiyo wakiongozwa na Mohammad bin Salman wakitumia fedha nyingi katika masuala ya kijeshi na vita vya kivamizi dhidi ya nchi nyingine.
Itakumbukwa kuwa, mwezi Machi 2015, Saudi Arabia kwa uungaji mkono wa Marekani, Imarati, utawala wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu, ilianzisha mashambulizi ya kivamizi ya pande zote dhidi ya nchi maskini ya Kiarabu ya Yemen na hadi hivi sasa zaidi ya watu 16 elfu wameshauawa na makumi ya maelfu ya wengine wameshajeruiwa. Mamilioni ya wananchi wa Yemen nao wamekuwa wakimbizi kutokana na uvamizi huo wa Saudi Arabia.