India yafunga kanali za televisheni za Kiislamu Kashmir
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57345-india_yafunga_kanali_za_televisheni_za_kiislamu_kashmir
India imepiga marufuku kurushwa matangazo ya kanali za televisheni za nchi za Kiislamu zikiwemo Iran, Uturuki na Malaysia katika eneo la Kashmir iliyo chini ya udhibiti wa serikali ya New Delhi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 18, 2019 08:04 UTC
  • India yafunga kanali za televisheni za Kiislamu Kashmir

India imepiga marufuku kurushwa matangazo ya kanali za televisheni za nchi za Kiislamu zikiwemo Iran, Uturuki na Malaysia katika eneo la Kashmir iliyo chini ya udhibiti wa serikali ya New Delhi.

Afisa wa Wizara ya Habari na Utangazaji ya India jana Jumapili aliyaagiza mashirika yanayohusika na upeperushaji wa mawimbi ya kanali hizo za televisheni katika eneo la Kashmir kufuata agizo hilo kikamilifu.

Huku akirejelea Sheria ya Urushaji Matangazo ya 1995, Vikram Sahay jana alikutana na wamiliki wa mashirika hayo katika mji wa Srinagar na kuwataka wasirushe matangazo ya kanali za nchi za Kiislamu zikiwemo Iran, Malaysia, Uturuki, Saudi Arabia, na Pakistan. 

Dhulma wanazopitia Waislamu wa Kashmir kila uchao

Haya yanajiri wakati huu ambapo maeneo mengi ya Kashmir yako gizani yasijue mambo yanayoendelea nje ya eneo hilo, baada ya serikali ya New Delhi kuyakatia mawasiliano ya simu na mitandao ya intaneti.

Aidha siku chache ziliopita, serikali ya India ilipiga marufuku sherehe zote za mazazi ya Mtume Muhammad (saw) pamoja na maadhimisho ya Wiki ya Umoja katika eneo hilo la Kashmir ambalo aghalabu ya wakazi wake ni Waislamu.