UN: Thuluthi moja ya wanawake wanakabiliwa na dhulma za kijinsia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i57486-un_thuluthi_moja_ya_wanawake_wanakabiliwa_na_dhulma_za_kijinsia
Umoja wa Mataifa umesema katika kila wanawake watatu, mmoja amekabiliwa na dhulma za kijinsia au kunajisiwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 25, 2019 08:42 UTC
  • UN: Thuluthi moja ya wanawake wanakabiliwa na dhulma za kijinsia

Umoja wa Mataifa umesema katika kila wanawake watatu, mmoja amekabiliwa na dhulma za kijinsia au kunajisiwa.

António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema hayo katika ujumbe wake kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Dhulma Dhidi ya Wanawake na Wasichana inayoadhimishwa leo Novemba 25.

Katika ujumbe huo, Guterres ametahadharisha kuhusu kuongezeka kwa visa vya kunyanyaswa na kudhulumiwa wanawake na wasichana kwa misingi ya jinsia zao, katika kona mbalimbali duniani.

Amesema, "Ongezeko la visa hivi linamaanisha kuwa, mtu aliye karibu nawe, iwe ni mtu wa familia, rafiki au mfanyakazi mwenzako ameathirika kwa njia moja au nyingine na unyanyasaji huu."

Wanawake wakiandamana Ufaransa kulalamikia unyanyasaji na dhulma dhidi yao

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, zaidi ya asilimia 50 ya vifo vya wanawake kote duniani vimetokana na dhulma hizi, huku aghalabu ya mauaji hayo dhidi ya wanawake yakifanywa na waume, wapenzi au watu wa familia. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) linasema kila siku, wanawake na wasichana 137 huuawa na jamaa zao. Wanaharakati wamefanya maandamano katika nchi kadhaa za Ulaya zikiwemo Ufaransa na Ubelgiji kulaani dhulma na unyanyasaji huo dhidi ya wanawake.