Mauzo ya silaha za Uingereza kwa muungano wa Saudia yaongezeka
https://parstoday.ir/sw/news/world-i58094-mauzo_ya_silaha_za_uingereza_kwa_muungano_wa_saudia_yaongezeka
Shirika la misaada ya kibinadamu la Oxfam limefichua kuwa, mauzo ya silaha za Uingereza kwa muungano vamizi wa Saudi Arabia katika mashambulizi ya Yemen yameongezeka kwa asilimia 50 ndani ya miaka mitano iliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 25, 2019 04:08 UTC
  • Mauzo ya silaha za Uingereza kwa muungano wa Saudia yaongezeka

Shirika la misaada ya kibinadamu la Oxfam limefichua kuwa, mauzo ya silaha za Uingereza kwa muungano vamizi wa Saudi Arabia katika mashambulizi ya Yemen yameongezeka kwa asilimia 50 ndani ya miaka mitano iliyopita.

Ripoti ya utafiti wa shirika hilo lenye makao makuu yake nchini Uingereza imebaini, serikali ya London imeuuzia muungano huo wa kijeshi wa Saudia silaha zenye thamani ya pauni bilioni 6.4  tokeo 2015, zikiwemo helikopta, makombora na ndege zisizo na rubani (drone).

Ruth Tanner, Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu wa Oxfam amelaani ongezeko hilo la uuzaji silaha unaofanywa na London, akisisitiza kuwa mauzo hayo ni doa katika hisia za upambanuzi za Uingereza, kwa kutilia maanani vita vinavyofanywa na wanunuzi dhidi ya Yemen.

Hali kadhalika shirika hilo la misaada ya kibinadamu la Oxfam limetahadharisha kuhusiana na kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu nchini Yemen.

Nchi 5 zinazoiuza Saudia silaha kwa wingi duniani

Shirika hilo limelaani jinai zinazoendelea kufanywa na muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia dhidi ya wananchi wa Yemen ikiwa ni pamoja na kuzuia kufikiwa na chakula, mafuta na madawa Wayemen licha ya wananchi hao kuwa na majanga yasiyoelezeka.

Ikumbukwe kuwa Marekani na nchi za Magharibi hasa Uingereza ndio wauzaji wakuu wa silaha zinazotumiwa na Saudi Arabia na wapambe wake kufanya jinai za kinyama nchini Yemen tokea mwaka 2015, ambapo hadi hivi sasa zaidi ya watu laki moja wameshauawa na makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa.