Wamarekani wenye asili ya Afrika wanapinga vikali kuendelea urais wa Trump
Uchunguzi wa maoni umebaini kuwa, idadi kubwa ya Wamarekani weusi, yaani Wamarekani wenye asilia ya Afrika wanatekeleza mikakati maalumu ya kuhakikisha kuwa Donald Trump hachaguliwi tena kuwa rais wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa na tovuti ya Axios, idadi kubwa ya wapiga kura katika jamii ya Wamarekani wenye asili ya Afrika wana hamu ya kupiga kura katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2020 ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2016.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, kumuondoa Donald Trump madarakani ndio sababu kuu ambayo imepelekea Wamarekani wenye asili ya Afrika wapate hamu kubwa ya kupiga kura katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2020.
Aidha uchunguzi huo umebaini kuwa, Wamarekani wenye asili ya Afrika wanaamini kuwa, upigaji kura ni njia bora zaidi ya kubainisha malalamiko yao kwa utawala wa Marekani.
Aidha kudorora uchumi ni sababu nyingine ambayo imepelekea Wamarekani wenye asili ya Afrika watake kupiga kura kwani matatizo yao yameongezeka tokea Trump aingie madarakani.
Axios imesema matokeo hayo ya uchunguzi wa maoni ni kengele ya hatari kwa Trump kwani itakuwa vigumu kwake kupata wapiga kura wenye asili ya Afrika.
Uchunguzi huo wa maoni pia umebaini kuwa kuna wapiga kura wapatao milioni 30 Wamarekani wenye asili ya Afrika ambao wanaweza kupiga kura katika uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika Novemba 3, 2020. Chama cha upinzani cha Democrat kimekuwa kikifanya kampeni maalumu za kuwavutia wapiga kura wenye asilia ya Afrika.
Trump ni maarufu kwa mitazamo yake ya kibaguzi kuhusu Waafrika au Wamarekani wenye asili ya Afrika na wahajiri, hasa Waislamu.