Maandamano dhidi ya sera ya kupenda vita ya Marekani yafanyika duniani
Maandamano yameshuhudiwa katika nchi mbalimbali duniani kupinga sera ya kupenda vita ya Rais Donald Trump wa Marekani sambamba na kupinga hatua yoyote ya Washington ya kuanzisha vita na Iran.
Maandamano hayo yaliyofanyika kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Uchukuaji Hatua yalishuhudiwa jana Jumamosi ndani ya Marekani kwenyewe na katika nchi kadhaa duniani kama vile Canada, Armenia na Uganda.
Mjini Washington, waandamanaji walikuwa wamebeba mabango yenye jumbe za kuitaka serikali ya Trump isithubutu kuanzisha vita dhidi ya Iran sambamba na kuitaka iviondoe vikosi vya jeshi la Marekani nchini Iraq. Mbali na mjini Washington, maandamano kama hayo yalifanyika pia katika miji mingine ya Marekani kama vile San Francisco, California, Madison na Wisconsin.
Mjini Toronto Canada na katika mji mkuu wa Uganda, Kampala waandamanaji wametoa mwito wa kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala Iran wakisisitiza kuwa hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu haitakuwa na matokeo mengine isipokuwa kulitumbukiza eneo zima la Asia Magharibi katika vita na ghasia.
Kadhalika wamekosoa vikali hatua ya Washington ya kuiwekea vikwazo Iran wakisisitiza kuwa vikwazo na mashinikizo ya kiuchumi ni aina fulani ya vita.
Mapema mwezi huu, maelfu ya wanaharakati na wananchi wa Marekani walifanya maandamano katika makumi ya miji ukiwemo mji mkuu Washington, kulaani hatua ya utawala wa Donald Trump ya kumuua shahidi kamanda wa jeshi la Iran, Luteni Jenerali Qassem Soleimani, pamoja na hatua ya Washington ya kutuma maelfu ya askari katika eneo la Asia Magharibi baada ya kutekeleza ukatili huo.