Wagombea wa urais Marekani wakosoa 'mpango wa amani' wa Trump
Wagombea wa chama cha Democrat kwenye uchaguzi wa rais wa mwaka huu 2020 nchini Marekani wamekosoa vikali kile kinachotajwa kuwa mpango wa amani uliozinduliwa hivi karibuni na Rais Donald Trump wakisisitiza kuwa, pendekezo hilo lililopewa jina la wa 'Muamala wa Karne' halitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kushadidisha mgogoro baina Palestina na Israel.
Seneta wa Vermont, Bernie Sanders amesema mpango huo haukubaliki, kwa kuwa mpango wowote wa amani unaokubalika sharti ufuate sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Sanders amesema mpango huo ulipaswa utamatishe ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Palestina sambamba na kufanikisha azma ya kuundwa taifa huru la Palestina, lakini mpango huo wa Trump uko mbali kabisa na uhalisia huo.
Naye Seneta wa Massachusetts wa chama cha Democrat, Elizabeth Warren amesema "Muamala wa Karne" wa Trump ni muhuri wa kuhalilisha kuendelea kuporwa na kukaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina na mpango huo hautoi fursa yoyote ya kuundwa taifa huru la Palestina.
Kwa upande wake, Joe Biden ambaye pia ni mmoja wa wagombea wa chama cha Democrat kwenye uchaguzi ujao wa rais nchini Marekani amesema mpango huo eti wa amani wa Trump ni mchezo wa kisiasa ambao utachelewesha zaidi mchakato wa amani.
Na Pete Buttigieg, Meya wa zamani wa Indiana na pia mmoja wa wanasiasa wanaotazamia kupeperusha bendera ya Democrats katika uchaguzi wa urais wa Marekani amesema, "mpango wa rais wa Muamala wa Karne, kama alivyofanya katika mambo mengine ya sera za nje, atasababisha suala tata kuwa tata zaidi."