Waziri Kiongozi wa Uttar Pradesh: Waislamu walishwe risasi badala ya biriani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i58984-waziri_kiongozi_wa_uttar_pradesh_waislamu_walishwe_risasi_badala_ya_biriani
Waziri Kiongozi wa jimbo la Uttar Pradesh nchini India kutoka chama cha Waziri Mkuu wa nchi hiyo ametoa matamshi ya kibaguzi na kichochezi dhidi ya Waislamu akitaka wauawe.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 06, 2020 08:55 UTC
  • Yogi Adityanath
    Yogi Adityanath

Waziri Kiongozi wa jimbo la Uttar Pradesh nchini India kutoka chama cha Waziri Mkuu wa nchi hiyo ametoa matamshi ya kibaguzi na kichochezi dhidi ya Waislamu akitaka wauawe.

Yogi Adityanath ambaye ni mashuhuri kwa kuhubiri chuki na machafuko dhidi ya Waislamu nchini India amewaambia watu wa jimbo hilo kwamba, Waislamu wanaoandamana kupinga sheria mpya ya uraia ni "magaidi" wanaopaswa kulishwa "risasi badala ya biriani".

Vilevile amewataja maelfu ya wanawake wanaoandamana katika kiunga cha Shaheen Bagh mjini New Delhi kuwa ni magaidi.

Sheria ya uraia, CAA kwa kifupi iliyopasishwa Disemba mwaka jana na kuungwa mkono na chama tawala cha Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi cha Bharatiya Janata Party (BJP), imekabiliwa na upinzani mkubwa wa ndani na nje ya India ikitajwa kuwa ni ya kibaguzi. Sheria hiyo inawabagua Waislamu wa India kwa sababu ya imani yao ya kidini. Watu wasiopungua 30 wameuawa katika maandamano ya kupinga sheria hiyo.

Waislamu wa India wakiandamana kupinga sheria mpya ya uraia

Sheria hiyo inaruhusu kupatiwa uraia wahajiri wa jamii za Wahindu, Mabudha na hata Wakristo wanaotokea katika nchi jirani za Pakistan, Bangladesh na Afghanistan, lakini inazuia kupewa uraia Waislamu wanaotoka katika nchi hizo.

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeitaja sheria hiyo kuwa ya kibaguzi. Wakosoaji wamesema kuwa sheria hiyo ni sehemu ya melengo machafu ya chama cha Bharatiya Janata (BJP) kwa ajili ya kuwafukuza nchini humo wafuasi wa dini ya Kiislamu.